Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Kenya kujenga makazi salama nchini Saudi Arabia kuwahifadhi raia wake waliodhulumiwa - Mwanzo TV

Kenya kujenga makazi salama nchini Saudi Arabia kuwahifadhi raia wake waliodhulumiwa

Kenya inalenga kuwalinda wafanyikazi wake dhidi ya dhuluma katika nchi za Mashariki ya Kati kwa kuanzisha mpango wa makazi salama katika nchi hizo.

Katibu wa Baraza la Mawaziri la Wafanyakazi Simon Chelugui alisema KSh70 milioni zimetengwa kujenga makazi salama nchini Saudi Arabia ambako wafanyakazi kutoka kenya wamepitia mateso ya kiakili na kimwili na ukiukaji wa haki zao.

Wafanyikazi wa nyumbani nchini Saudi Arabia mara nyingi huripotiwa kuwa waathiriwa wa dhuluma na ukatili kutoka kwa waajiri wao.

Visa vinavyoripotiwa ni kati ya mateso ya kisaikolojia hadi ya kimwili, huku baadhi yao wakifariki.Serikali pia imeanza kufuatilia Wakenya wanaoteseka nje ya nchi huku ikiweka hatua kali kudhibiti wahamiaji haramu wanaofanya kazi kinyume cha sheria katika nchi hizo.

Waziri Chelugui alisema sasa itakuwa lazima kwa mawakala wote wa kuajiri kusajiliwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Uajiri (NEA) ili waruhusiwe kusafirisha vibarua.

Akizungumza mjini Mombasa wakati wa uzinduzi rasmi wa Maonyesho ya Kitaifa ya Waajiri, Waziri alisema afisi yake itafanya kazi pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani na washikadau wengine kuhakikisha kuna utiifu katika kuajiri wakenya kwenda mataifa ya nje.

“Tutatekeleza sharti kwamba waajiri wote wa kibinafsi wasajiliwe na NEA waruhusiwe kuajiri Mkenya yeyote kufanya kazi nje ya nchi.”

“Kama hatua ya haraka ya kuwaokoa wale wanaoteseka nje ya nchi na zaidi nchini Saudi Arabia, tutaanzisha makazi salama ili kuwalinda wale wanaodhulumiwa tunapopanga kuwarejesha makwao, “alisema Bw Chelugui.

“Baadhi ya mawakala wamechukua fursa ya mapungufu ya kisera ili kuwanyanyasa Wakenya lakini sasa kwa sera hizo mpya, watalazimika kuzizingatia la sivyo watafunga ofisi zao,” akasema.

Waziri huyo alitaja eneo la Pwani kuwa mojawapo ya maeneo yenye idadi kubwa ya mawakala wa kuajiri watu ambao hawajasajiliwa huku baadhi yao wakitumiwa kuwasajili vijana katika vikundi vya ugaidi.

“Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, tumesajili kesi 97 za Wakenya waliofariki wakifanya kazi nje ya nchi lakini tunataka kukomesha hilo,” ilisema data ya Kamati ya Bunge ya Kazi na Ustawi wa Jamii inaonyesha idadi ya Wakenya wanaofanya kazi na wanaoishi Saudi Arabia ilipanda kutoka 55,000 mwaka wa 2019 hadi 97,000 mwaka huu.