Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Kenya: Kundi la kwanza la wauguzi waliopata ajira Uingereza tayari kusafiri - Mwanzo TV

Kenya: Kundi la kwanza la wauguzi waliopata ajira Uingereza tayari kusafiri

Kundi la kwanza la wauguzi wa Kenya walioajiriwa kufanya kazi nchini Uingereza wanatarajiwa kuondoka nchini kuelekea kituo chao kipya cha kazi siku ya Jumanne kama sehemu ya makubaliano ya nchi mbili kati ya Kenya na Uingereza kuhusu kuajiri wafanyikazi wa Afya.

Wauguzi hao kumi na tisa wameajiriwa katika hospitali ya kifahari ya Chuo Kikuu cha Oxford huku 13 kati yao wakiondoka siku ya Jumanne huku 6 waliosalia wakiondoka katika muda wa wiki mbili baada ya kukamilika kwa shughuli ya kuwaidhinisha.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga wauguzi, waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema wauguzi wengine 80 waliohitimu tayari wamefaulu mtihani huo na kwa sasa wanangojea kukaguliwa na kuna uwezekano wa kupelekwa katika hospitali zingine nchini Uingereza.

Alipongeza jukumu lililochukuliwa na wauguzi kote ulimwenguni kuelekea kufikiwa kwa huduma bora ya afya kwa wote.

“Wauguzi ndio kiini cha afya ulimwenguni, kutoka kwa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na ya kuambukiza, hadi kushughulikia dharura za kiafya na kuzuia milipuko.”

Huku Kenya ikiwa imepokea maombi kadhaa kutoka mataifa tofauti kuwaajiri wauguzi wa Kenya, Kagwe alisema Wizara ya Afya itaunda kikosi kazi kushughulikia uajiri wote wa kimataifa kwa wafanyakazi wa afya nchini.

“Kwa sasa tumepokea maombi kadhaa kutoka mataifa tofauti kwa wauguzi wa Kenya.

Hii italazimu kuwepo kwa utaratibu wa kusimamia mchakato huo kwani pia tunakagua na kudhibiti uhaba wa wauguzi na wakunga waliosalia nchini.” Alisema waziri wa afya.

Alichukua nafasi hiyo kumpongeza Mercy Wasike, muuguzi wa Kenya ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Muuguzi Mkuu katika Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza, na kuwataka wanaosafiri kwenda Uingereza kuwa mabalozi wazuri wa Kenya.

Alisema makubaliano kati ya serikali ya Kenya na Uingereza yanaruhusu zaidi ushirikiano mzuri katika mitazamo mingine mingi katika sekta ya afya ikiwemo elimu na maendeleo endelevu ya kitaaluma.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kamishna Mkuu wa Uingereza nchini Kenya Jane Marriot alisema kuwa kuajiri wauguzi hao ni hatua muhimu katika utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano wa wafanyikazi wa afya.

“Huku wauguzi wa Kenya na wahudumu wa afya kwa ujumla wakifanya kazi katika NHS kwa miongo kadhaa, leo ni mwanzo wa enzi mpya ya kuajiri wauguzi wa kimataifa nchini Uingereza kupitia mpango wa serikali hadi serikali.”Alisema Marriot.

Alisema mpango huo utapanuka zaidi hadi kada zingine za wafanyikazi wa afya akiongeza kuwa Kenya inapaswa kuweka mfumo wa kutuma maombi ili kukidhi mahitaji makubwa yanayotarajiwa kutoka Uingereza na mataifa mengine.

Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ni Waziri wa Afya Susan Mochache na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dk. Patrick Amoth.

Makubaliano kati ya Kenya na Uingereza kuhusu kuajiri wafanyikazi wa Afya yalitiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson mnamo Januari 2021.