Mawakili wa aliyekuwa mgombea wa Azimio la Umoja Raila Odinga na aliyekuwa mgombea mwenza Martha Karua wameibua maswali mazito wakijaribu kuonyesha kuwa fomu za 34A katika sava za tume ya IEBC ziliitilafiwa na Jose Camargo, mmoja wa raia watatu wa Venezuela waliokamatwa na kufurushwa nchini Kenya.
Mawakili Paul Mwangi na Julie Soweto wameonyesha mahakama ya juu jinsi fomu moja ya 34A waliopata katika sava ya IEBC ilivyobadilishwa deta muhimu ikiwemo idadi ya kura.
Mwangi ameionyesha mahakama fomu moja ya 34A ilioandikwa jina Jose Camargo juu upande wa kushoto.
Camargo Castellano Jose Gregorio alikamatwa pamoja na Joel Gustavo Rodriguez Garcia na Salvador Javier Suarez siku ya alhamisi, Julai 21 wakati wakisafirisha stakabathi muhimu za uchaguzi.
Watatu hao baadaye walisemekama kuwa wafanyikazi wa kampuni ya Kitaifa ya Smartmatic BV, ambayo ilipewa kandarasi na IEBC kuwasilisha teknolojia ya kutumika wakati wa uchaguzi wa agosti tisa.
“Tunaamini kuwa hizo ni alama za vidole za mmoja wa watuhumiwa wa wizi katika uchaguzi huu,” alisema wakili Mwangi.
Wakati wa kujibu waswali yalioibuka, wakili Soweto alifanikiwa kupakua fomu 34A ya kituo cha shule ya msingi ya Gicharaigu ilioko eneo la Kangema kutoka kwa tovuti ya IEBC.
“Tukiangazia sasa fomu 34A, juu upande wa kushoto wa fomu hiyo kuna jina ya raia wa kigeni Jose Camargo, tumeambiwa hakukuwa raia wa kigeni katika uchaguzi huu, tumeambiwa raia hao wa kigeni waliondoka nchini kabla ya agosti nane, tumeambiwa kuwa hawakuwa na ufunguo wa sava,’ alisema Soweto
“Raia huyu wa Venezuela kwa jina Jose Camargo ndiye aliyefanya uamuzi kuhusu rais mteule wa taifa la Kenya, huyo ndiye aliyeitilafiana na matokeo ya uchaguzi wa urais.” Aliendelea wakili Soweto
Wakili Soweto pia alizua maswali kuhusu stemp ya IEBC katika fomu ambayo alisema ilifanana na aliyoipakua katika mtandao wa IEBC na ilikuwa vilevile na alama za kuitilafiwa na idadi ya kura kubadilishwa.
“Tunapojumuisha idadi ya kura, tunapata 316, idadi jumla ya kura zilizopigwa kulingana na fomu hiyo ni 321 ambayo ni tofauti na tulioona. Kura zilizoharibika ni 4, hii ina maana kuwa kulingana na hesabu, kuna shida tayari,” alisema wakili Soweto.
Pia alizua maswali kuhusu mitambo ya KIEMS ambapo alipakua fomu 34A kutoka maeneo ya Mt. Elgon na Nyeri ambayo yalikuwa na nambari ya usajili iliyofanana, F230450M00204133.