#KENYA: Nahodha wa zamani wa kandanda, Victor Wanyama kurejea katika timu ya taifa

Victor Wanyama wakati wa mkutano wake na Waziri wa Michezo Ababu Namwamba

Nahodha wa zamani wa kandanda wa Kenya Victor Wanyama anasema kuwa ameamua kurejea katika kikosi cha taifa, zaidi ya mwaka mmoja tu baada ya kutangaza kustaafu soka ya kimataifa.

Kiungo huyo wa zamani wa Tottenham mwenye umri wa miaka 31 alisema ameamua kurejea Harambee Stars baada ya kukutana na Waziri wa Michezo wa Kenya Ababu Namwamba Jumatano.

“Nina furaha kutangaza kwamba nimekubali mwaliko wa waziri wa kurejea Harambee Stars,” Wanyama alisema.

Uamuzi wake huo unafuatia kuondolewa kwa marufuku ya FIFA kwa shirikisho la soka la Kenya ambalo hivi majuzi lilirejeshwa na serikali baada ya kuvunjwa kwa madai ya ufisadi.

“Ninaamini sote tuna jukumu la kupeleka soka ya Kenya mbele baada ya kurejea katika soka ya kimataifa,” Wanyama alisema. Nahodha huyo alikuwa ametangaza kustaafu mnamo Septemba 2021.

Namwamba alipongeza kurejea kwa Wanyama katika timu hiyo, akiandika kwenye Twitter: “Katika dhamira yetu ya kujenga upya kandanda yetu na kuinua timu zetu za kitaifa, wachezaji wetu mashuhuri lazima wawe kiini cha ufufuo huu.”

Wanyama ndiye mwanasoka wa kwanza Mkenya kucheza katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Alijiunga na klabu ya Ligi Kuu ya Soka ya Montreal mnamo Machi 2020 kwa uhamisho wa bure kutoka Tottenham na hapo awali alikuwa na Celtic na Southampton.