Search
Close this search box.
East Africa
Raila Odinga,muaniaji wa kiti cha rais

Kiongozi wa chama cha ODM na muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga amezindua wimbo wake ‘Leo ni Leo’.

Raila Odinga anapangia kutumia wimbo huo katika kampeini zake za urais mwaka huu. Uchaguzi mkuu nchini Kenya utafanyika Agosti 9.

Wimbo huo umetolewa rasmi leo kupitia mitandao ya kijamii na unamshirikisha msanii Emmanuel Musindi ambaye alikuwa mtunzi wa wimbo huo kabla kusmshirikisha Raila katika toleo la pili la wimbo huo.

“Leo ni Leo,” umepokelewa vyema na watu wengi katika mitandao ya kijamii. Katika video ya wimbo huo, Raila anaonekana akicheza na wanadensi na kucheza mpira.

Si mara ya kwanza kwa Raila Odiga kutumia nyimbo kupamba kampeni zake za urais.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2002, vyama vya NAC chake Charity Ngilu na Liberal Party of Kenya chake Raila Odinga vilikuja pamoja na kuunda muungano wa NARC. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo, chama cha NARC kilitumia wimbo “unbwogable” katika kampeini zao.

Wimbo huo ulikuwa utunzi wa wasanii Gidi Gidi na Maji Maji.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017, Raila Odinga tena alitumia wimbo katika kampeni zake za uchaguzi alipokuja pamoja na wanasiasa wenzake, Kalonzo Musyoka , Moses Wetangula na Musalia Mudavadi katika muungano wa NASA. Wakati huo walitumia wimbo wa “Raila Tibim” ulioimbwa na Onyi Jalamo.

Tofauti na nyimbo zilizotumiwa awali,Raila Odinga wakati huu amejumuishwa katika wimbo huo na msanii mtunzi wa wimbo Emmanuel Musindi ambaye ni mwanamuziki maarufu wa mtindo wa Benga kutoka magharibi mwa Kenya.

Wakenya wengi sasa wanasubri kuona iwapo muungano wa Kenya kwanza unaojumuisha wanasiasa William Ruto wa UDA, Moses Wetangula wa Ford Kenya na Musalia Mudavadi wa ANC kama watatoa wimbo wa kampeini. 

Comments are closed