Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amewasilisha rufaa katika Mahakama ya Afrika Mashariki kupinga uamuzi wa Mahakama ya Juu zaidi kwa kuunga mkono kuondolewa kwake kuwania ugavana jijini Mombasa.
Rufaa ya kutaka kuchunguzwa upya kwa kesi hiyo ilitokana na uamuzi wa mahakama ya majaji saba iliyotolewa Ijumaa wiki jana. Sonko kupitia kwa mawakili wake Kenneth Wanyanga na Danstan Omari alisema kwamba hakupewa nafasi ya kusikilizwa inavyotakiwa kisheria.
Alisema kuwa mahakama ya juu zaidi nchini haikuzingatia kwamba rufaa yake ya kuondolewa mashtaka haikujibiwa.
Wakati wa kusikilizwa kwa rufaa hiyo Sonko ataomba mahakama itoe maagizo ya muda ya kusitisha utekelezaji wa hukumu hiyo.
Aidha aliteta kuwa Mahakama ya Juu haikufutilia mbali agizo lililotolewa na majaji watatu wa Mahakama Kuu iliyoketi Mombasa iliyoagiza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kujumuisha jina lake katika orodha ya wagombezi.
Mawakili hao walisema kuwa mahakama ya Juu ilitoa uamuzi kuamuru kwamba shauri hilo lilipaswa kusikilizwa na majaji watano lakini majaji hao saba walifanya uamuzi wao wenyewe.
Mawakili hao pia walifichua kuwa wamewasilisha kesi mbele ya Mahakama ya Juu wakitaka kusitishwa kwa uamuzi huo.
Walisema kuwa Mahakama ya Juu imekiri kuwa haina mamlaka ya kusikiliza maombi ya mashitaka, badala yake waliendelea kutoa uamuzi.