Ripoti mpya ya Freedom House imebainisha kuongezeka kwa vitendo vya ukandamizaji wa kimataifa, ikisema serikali nyingi duniani zimeendelea kuwanyanyasa wakosoaji na wanaharakati hata nje ya mipaka yao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, “Mwaka uliopita, serikali mbalimbali duniani ziliwaua, kuwapiga, kuwateka nyara, kuwatisha na kuwanyanyasa wakosoaji nje ya mipaka yao.” Shirika hilo lilirekodi jumla ya matukio mapya 126 ya ukandamizaji wa moja kwa moja katika mwaka 2025 pekee, na kuongeza idadi ya visa vilivyokusanywa kwenye hifadhidata yake, ambayo inahusu kipindi cha 2014 hadi 2025, hadi kufikia 1,375
Kenya, Tanzania na Uganda yametajwa miongoni mwa mataifa yanayoshiriki katika ukandamizaji wa wapinzani na wanaharakati nje ya mipaka yao, ikionyesha Afrika Mashariki kama kitovu cha mashirikiano ya kiusalama yenye sura ya kiimla, kulingana na ripoti mpya ya Freedom House.
Ripoti hiyo inasema: ‘Mamlaka za Kenya, Uganda na Tanzania walishirikiana kufuatilia, kuwakamata na kuwarejesha wanaharakati kwa lengo la kuzuia kuhamasishwa kwa wananchi kabla na wakati wa uchaguzi. “Serikali za Afrika Mashariki zimezidi kushirikiana katika kuwashambulia na kuwalenga wanaharakati nje ya mipaka”, iliongeza sehemu ya ripoti hiyo.
Kenya ilihusishwa moja kwa moja na tukio la Novemba 2024 ambapo kiongozi wa upinzani wa Uganda, Kizza Besigye, alitoweka jijini Nairobi alipohudhuria uzinduzi wa kitabu. Baada ya awali kukanusha, Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi alikiri kushirikiana na maafisa wa Uganda, akitaja “maslahi ya kitaifa” na uhusiano wa kibiashara kama sababu za operesheni hiyo.
Uganda imetajwa kuwa na zaidi ya matukio 40 ya ukandamizaji wa kimataifa tangu 2014. Ripoti hiyo imedai kuwa mara nyingi imekuwa ikishirikiana na Kenya na Tanzania kufuatilia na kuwarejesha wapinzani.
Tanzania iliingia rasmi kwenye orodha ya wahusika mwaka 2025. Tukio kubwa lilihusisha utekaji wa muda wa mwanaharakati Maria Sarungi Tsehai jijini Nairobi, ambapo alidai kushambuliwa na maafisa wa usalama wa Tanzania.
“Walimpiga na kujaribu kufungua simu yake. Tsehai ni mpiga filimbi na mwanaharakati wa uhuru wa kujieleza ambaye alikimbia Tanzania mwaka 2020 kutokana na vitisho dhidi yake. Harakati yake ya kisiasa, Change Tanzania, iliwalaumu maafisa wa usalama wa Tanzania kwa shambulio hilo la kuvuka mipaka.” ilisema ripoti hiyo
“Mwezi Oktoba, Rais Samia Suluhu Hassan alichaguliwa tena katika uchaguzi ulioelezewa kuwa na dosari kubwa, uliosheheni vurugu dhidi ya waandamanaji wa amani.” ilieleza Freedom House
Pia, wanaharakati wa Kenya na Uganda walikamatwa na kufukuzwa walipokuwa wakifuatilia kesi ya upinzani dhidi ya Tundu Lissu.
“Mwezi Julai, Mwabili Mwagodi, mshiriki mwenye sauti kubwa katika maandamano ya Gen Z ya mwaka 2024 nchini Kenya, alitoweka kwa muda jijini Dar es Salaam, Tanzania, muda mfupi baada ya kukosoa mtandaoni maafisa wa usalama wa Kenya. Tukio hilo lilijiri miezi miwili tu baada ya mamlaka za Tanzania kuwapiga na kisha kuwafukuza wanaharakati kadhaa wa Kenya na Uganda pamoja na maafisa wa zamani wa serikali” iliandika ripoti hiyo
Kulingana na Freedom House mashirikiano haya ya kikanda yanapunguza nafasi za mshikamano wa kiraia na yanawasaidia viongozi walioko madarakani kuzidisha nguvu zao wakati wa uchaguzi, hali inayozua maswali makubwa kuhusu heshima ya haki za binadamu katika ukanda wa Afrika Mashariki.