Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Jumanne imeahirisha kusikizwa kwa kesi ya Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a Sabina Chege hadi Machi 8 kufuatia kulazwa kwake hospitalini.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Utekelezaji wa Maadili ya Uchaguzi ya Tume hiyo, Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema kuwa Chege pia anapaswa kujiepusha kutoa maoni yake kuhusu kesi hiyo katika vikao vya umma.
Kusikizwa kwa kesi ya Chege kuhusu matamshi yake ya wizi wa kura kuliahirishwa kutokana na ombi la wakili wake Otiende Amollo.
Katika ombi lake Amollo alisema kuwa mteja wake ni mgonjwa na amelazwa katika Hospitali ya Nairobi ambako amekuwa akipokea matibabu tangu tarehe 16 Februari 2022. Wakili alieleza yaliyokuwemo kwenye barua ya Dkt Eric Munene Muriuki alibainisha kuwa haikuwa wazi ni lini Chege angeruhusiwa kutoka hospitalini.
Alisema kuwa matokeo ya kura za mwaka 2017 hayakuwa sahihi kutokana na wizi wa kura uliofanyika wakati huo na hali hiyo hiyo inaweza kutokea katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.
Mara moja alikanusha kutamka maneno hayo akisema alinukuliwa vibaya.
Siku ya Jumanne jioni, Kinara wa muungano wa Azimo la Umoja Raila Odinga na viongozi wengine walimtembelea Sabina Chege hospitalini alikolazwa.
Odinga na wanasiasa wengine walikuwa wametoka katika ziara ya muungano wa Azimio la Umoja maeneo ya pwani ambako walifanya mikutano maeneo ya Lamu na Taita Taveta.