Search
Close this search box.
East Africa

Uingereza na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini humo wameeleza imani yao kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwezi ujao utakuwa huru na wa amani.

Mjumbe wa Uingereza Jane Marriot alisema nia ya kimsingi ya serikali yake ni kwamba Kenya iwe na utulivu na ustawi zaidi.

“Macho ya ulimwengu yanaiangalia Kenya, na marafiki wa Kenya wanaendelea kupatikana ili kusaidia raia na Serikali ya Kenya katika maandalizi yake ya uchaguzi wa Agosti. Nina imani kuwa kupitia mkutano huu, kutakuwa na dhamira mpya ya washikadau wote kujitolea kuwepo kwa uchaguzi huru, wa haki, wa kuaminika na wa amani,” Marriot alisema katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Kongamano la Kitaifa la Uchaguzi (NEC) katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta Jumatatu.

Alisema, wanafuatilia kwa karibu vitendo vya viongozi na wanasiasa kwani alibainisha kuwa wale wanaochochea vurugu au kudhoofisha demokrasia wanapaswa kuwajibika kwa matendo yao.

Marriot alisema kuwa taifa lake halitaegemea upande wowote na halina ajenda ila kusaidia kuhakikisha watu wa Kenya wanakuwa na uchaguzi wenye mafanikio.

“Wakati fulani watu bado wananiuliza, nini ajenda ya kweli ya Uingereza, ni ajenda gani fiche ya Uingereza katika uchaguzi wa Kenya. Nataka nieleweke wazi kwamba yeyote atakayechaguliwa na wakenya ni suala la watu wa Kenya. Uingereza inaheshimu uhuru wa Kenya na hatupendelei upande wowote.” alisema.

Balozi wa EU nchini Kenya Henriette Geiger kwa upande wake alisema IEBC, inafaa kuruhusiwa kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kuendesha uchaguzi.

“Kenya ni nchi ya kipaumbele kwa uungwaji mkono na EU, ikiwa ni pamoja na uchaguzi kwa sababu Kenya ni muhimu. Kinachotokea hapa Kenya ni muhimu sana kwa ulimwengu. Ninaamini kusainiwa kwa Ahadi ya Amani ya Uchaguzi labda ni wakati muhimu zaidi katika mchakato wa uchaguzi,” mjumbe wa EU alisema

Comments are closed