Mahakama ya upeo imeidhinisha kwa kauli moja uchaguzi uliotangazwa na tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC kumtangaza rais mteule William Ruto kama mshindi wa uchaguzi wa agosti.
“Tunatangaza kuwa kuchaguliwa kwa William Ruto kama rais mteule kama uliowa huru na haki,” alisema Jaji mkuu Martha Koome.
Jaji mkuu akiwasilisha uamuzi huo wa majaji wote saba, amesema walalamishi walifeli kutoa ushahidi wa kutosha kuwa kulishuhudiwa makosa na ukiukaji wa sheria yalioweza kupelekea uchaguzi huo kufutiliwa mbali.
“Tumekubaliana na tunatangaza kuwa rais mteule alipata asilimia 50 na kura moja ya kura zote zilizopigwa kulingana na kipengee cha 138.4 cha katiba,” alisema jaji mkuu.
Mahakama kuu vilevile imetupilia mbali kesi zingine zilizowasilishwa mbele yake zikitaka kuchaguliwa kwa William Ruto kama rais mteule kufutwa.
Jaji mkuu akijibu maswala yaliowasilishwa mbele yake na muungano wa Azimio la umoja, amesema majaji hawakuwashawishi vya kutosha kwamba teknolojia ilifeli katika majaribio ya uadilifu, uthibitisho, usalama na uwazi.
Kuhusu suala kuwa kulikuwa na kuingiliwa kwa matokeo kama yalivyopakiwa kwenye tovuti ya tume ya uchaguzi.
Majaji wamesema kuwa hakuna ushahidi kwamba mfumo wa matokeo uliingiliwa
Jaji mkuu pia katika uamuzi huo amesema hakukuwa na ushahidi kwamba fomu za uchaguzi katika tovuti ya IEBC zilibadilishwa kutoka fomu za awali zilizochapishwa.
Jaji Koome amekosoa baadhi ya waliowasilisha hati za kiapo na akawaonya mawakili dhidi ya kuwasilisha ushahidi duni na potovu mahakamani.
Jaji mkuu alisema kuahirishwa kwa baadhi ya chaguzi hakukuwa na ukandamizaji wa wapiga kura na kumdhuru Raila Odinga.
Tume ya uchaguzi ilikuwa na uwezo wa kuahirisha uchaguzi katika baadhi ya maeneo
Kwa hivyo Mahakama ya Juu imeridhika kwamba tume ya uchaguzi ilikuwa na uwezo wa kuahirisha uchaguzi katika baadhi ya sehemu za nchi.