Mjadala wa manaibu Rais utafanyika Jumanne, Julai 19 katika Chuo Kikuu cha Catholic University of East Africa (CUEA) huko Karen, Nairobi.
Mdahalo utafanyika kwa awamu mbili huku wa kwanza ukijumuisha wagombea wa Naibu Rais ambao ukadiriaji wa umaarufu wao, kulingana na kura tatu za maoni za hivi majuzi, upo chini ya 5% awamu ya pili itahusisha wagombea ambao umaarufu wao katika kura za maoni ni zaidi ya 5% katika tafiti sawa za maoni.
Mjadala wa kwanza utaanza saa 6:00 jioni na kumalizika saa 7:30 jioni huku mdahalo wa pili ukianza saa 8:00 usiku hadi saa 9:30 usiku.
Kuwahusu wagombea wenza
Justina Wambui Wamae
Bi Justina Wambui Wamae ni mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 35 aliyegeuka kuwa mwanasiasa na ni mgombea mwenza wa Prof. George Wajackoyah wa Roots Party.
Alichaguliwa kuwa mgombea mwenza baada ya kuomba nafasi hiyo kwa kutumia wasifu aliotumia kuomba nafasi ya kuwa Katibu Mkuu Kiongozi baada ya uchaguzi mwaka 2017.
Alisoma katika Chuo Kikuu cha Daystar, na kuhitimu mwaka 2010 na Shahada ya Kwanza katika Management Information Systems.
Mwaka 2012 alihitimu na Diploma katika Purchasingand Supply Chain Management kutoka Chuo Kikuu cha Chartered Institute of Procurement and Supplies UK
Mwaka 2014 alihitimu na Shahada ya Uzamili ya Purchasing and Logistics kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT)
Ruth Mucheru Mutua
Ndiye mgombea mwenza wa David Mwaure Waihiga wa Agano Party.
Yeye ni mtaalam wa mawasiliano
Alisomea katika shule ya msingi ya State House
Shule ya upili ya Visa Oshwal
Alipata Diploma kutoka chuo cha Kenya Institute of Business Training mwaka wa 2004
Alipata shahada katika Communication and Sociology kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka wa 2010
Geoffrey Rigathi Gachagua
Rigathi Gachagua alizaliwa mwaka wa 1965 katika kijiji cha Hiriga eneo bunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri, akiwa mtoto wa nane kwa Nashashon Gachagua Reriani na Martha Kirigo.
Wazazi wake walikuwa wapiganaji wa Mau Mau katika msitu wa Mt.Kenya ambapo Nashashon Gachagua Reriani alikuwa akihudumia wapiganaji hao.
Alijiunga na Shule ya Msingi ya Kabiruini kuanzia 1971 hadi 1977 kabla ya kuendelea na Shule ya Upili ya Kianyaga kwa kiwango cha O-level na A-level.
Mnamo 1985, alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo alihitimu na Shahada ya Arts and Political Science and Literature in 1988 mnamo 1988.
Alimuoa Dorcas Wanjiku Rigathi, ambaye ni mchungaji anayeishi Mathira.
Baada ya kuhitimu, Gachagua aliajiriwa kwa muda mfupi katika Wizara ya Mambo ya Ndani na Urithi wa Kitaifa wa Kenya kabla ya kujiunga na Taasisi ya Polisi ya Utawala mnamo 1990.
Baada ya kuhitimu kutoka Taasisi ya Polisi ya Utawala, Gachagua aliwekwa katika Ofisi ya rais wa wakati huo Daniel Arap Moi kama Kadeti ya Afisa wa Wilaya kati ya 1991 na 1992.
Gachagua alichaguliwa kuwa mbunge wa eneo bunge la Mathira nchini Kenya mwaka wa 2017 kwa tiketi ya Jubilee.
Martha Wangari Karua
Martha Wangari Karua aliyezaliwa 22 Septemba 1957 alikuwa mbunge wa muda mrefu wa eneo bunge la Gichugu na ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya.
Alikuwa Waziri wa Sheria hadi alipojiuzulu kutoka wadhifa huo Aprili 2009. Karua aliwania urais mwaka wa 2013 chini ya tikiti ya Narc-Kenya na kumfanya kuwa mwanamke wa tatu kuwania wadhifa wa juu zaidi, baada ya Charity Ngilu na Wangari Maathai katika uchaguzi wa 1997.
Aliibuka wa sita katika kinyang’anyiro hicho.
Alisomea shule ya msingi ya Mugumo baadae Shule ya Wasichana ya St Michael’s Keruguya.
Kisha aliendelea na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kiburia, shule ya upili ya Wasichana ya Ngiriambu, na shule ya upili ya Wasichana ya Karoti.
Kisha alisoma shule ya upili ya Nairobi Girl kwa viwango vya A.
Alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi kuanzia 1977 hadi 1980. Kati ya 1980 na 1981 alisajiliwa katika Shule ya Sheria ya Kenya kwa kozi ya sheria ya shahada ya uzamili.
Karua aligombea uchaguzi wa urais wa Kenya wa 2013, chini ya tikiti ya chama cha NARC Kenya, aliibuka wa sita kwa kura 43,881.
Martha Karua alirejea katika ulingo wa kisiasa nchini Kenya katika uchaguzi mkuu wa 2017 akiwania Kiti cha Ugavana katika Kaunti ya Kirinyaga.
Alishindwa na Gavana wa sasa Anne Waiguru katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali baada ya kupata kura 122, 091 dhidi ya kura 161,373 za Bi Waiguru.