Kenya yaadhimisha miaka 61 ya kuwa Jamhuri

Kenya imeadhimisha miaka 61 tangu kuwa Jamhuri.

Siku ya Jamhuri ni sikukuu ya kitaifa nchini Kenya, inayoadhimishwa tarehe 12 Disemba kila mwaka.

Hiyo ndiyo siku rasmi ambayo Kenya ilipata kuwa nchi huru mnamo Disemba 12, 1963, miezi sita na siku kumi na moja baada ya kupata utawala wa ndani mnamo 1 Juni 1963 (Siku ya Madaraka) kutoka Uingereza.

Kenya baadaye ikawa Jamhuri, na kuapishwa kwa Jomo Kenyatta kama Rais kulifanyika tarehe 12 Disemba 1964, mwaka mmoja kamili baada ya Kenya kupata uhuru mwaka 1963.

Kenyatta, akiwa ameapishwa awali kama Waziri Mkuu, aliendelea kuwa Waziri Mkuu wa Kenya mpya, kabla ya kushika wadhifa wa rais mwaka mmoja baada ya Siku ya Uhuru.

“Leo tunathibitisha kwa kutafakari yale tuliyotimiza tangu kuinua bendera ya taifa letu, kwamba kwa kubaki waaminifu kwa utambulisho wetu wa kitaifa, tumebaki thabiti katika misimu ya wingi na uhaba. Katika wakati wetu, kizazi chetu hakipaswi kamwe kusahau tulipokuwa miongo sita iliyopita. Hatupaswi kupuuza ukweli kwamba uhuru, demokrasia na maendeleo yetu yalipatikana kupitia michango ya mamilioni ya wazalendo waliodhamiria,” rais Willim Ruto alisema akiongoza sherehe za kuadhimisha siku hii katika uwanja Uhuru Gardens jijini Nairobi.

Rais wa Gambia Adama Barrow alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo.

“Tangu uhuru, Kenya imeendelea kuongoza katika utawala wa kidemokrasia, amani na usalama. Kama mhusika mkuu katika ushirikiano wa Afrika, mbinu za nchi katika mabadiliko ya hali ya hewa na maendeleo hutumika kama mfano kwa wengine.”

Rais Ruto alichukua fursa hii kukashifu kile alichoita upinzani potofu.