Kenya yaanzisha uchunguzi wa vifo vya ‘madhehebu ya njaa’

Wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi mnamo Jumatatu walianza zoezi la uchunguzi wa zaidi ya maiti mia moja zilizopatikana kwenye makaburi ya halaiki zilizohusishwa na mhubiri wa Kenya anayedaiwa kuwachochea wafuasi wake kufa kwa njaa.

“Shughuli ya uchunguzi wa miili hiyo inaanza mara moja,” Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki aliwaambia waandishi wa habari nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali katika mji wa pwani wa Malindi.

“Tuko hapa kushuhudia hatua muhimu sana,” alisema. “Mchakato huo unatarajiwa kuchukua takriban wiki, yote yanakwenda vizuri.”

Wachunguzi pia watachukua sampuli za DNA kusaidia utambuzi, ingawa matokeo kamili yanaweza kuchukua miezi, daktari mkuu wa serikali, Johansen Oduor, alisema.

Makaburi ya watu wengi katika msitu ulio karibu wa Shakahola yamefichua watu wengi waliofariki, wengi wao wakiwa watoto.

Lakini idadi ya vifo ya 109, ambayo inajumuisha idadi ndogo ya watu ambao walipatikana wakiwa hai lakini walikufa wakiwa njiani kupelekwa hospitalini, bado ni ya muda.

“Taratibu za ufukuaji zilisitishwa kwa muda kwa sababu wataalamu walitushauri kuwa mvua inaponyesha mchakato huo hauwezi kuendelea,” Kindiki alisema.

Paul Mackenzie Nthenge, dereva wa zamani wa teksi ambaye alianzisha dhehebu la Kikristo liitwalo Good News International Church, anashutumiwa kwa kuwaambia wafuasi kwamba njaa inatoa njia kwa Mungu.

Lakini Kindiki alisema Ijumaa kuwa ripoti za awali zilidokeza “kwamba baadhi ya wahasiriwa huenda hawakufa kwa njaa. Kulikuwa na mbinu nyingine zilizotumika, ikiwa ni pamoja na kuwaumiza.”

Kugunduliwa kwa miili hiyo kulishtua sana Kenya, athari iliyoongezwa wiki iliyopita na tangazo kwamba mwinjilisti mashuhuri atashtakiwa kwa “mauaji ya watu wengi” ya wafuasi wake.

Ezekiel Odero, mkuu wa kanisa la New Life Prayer Center and Church, ambaye alikamatwa siku ya Alhamisi, anashukiwa kwa uhalifu ikiwa ni pamoja na mauaji, kusaidia kujiua, utekaji nyara, itikadi kali, uhalifu dhidi ya ubinadamu, ukatili wa watoto, ulaghai na utakatishaji fedha.

Mwendesha mashtaka Peter Kiprop alisema wiki jana kwamba kulikuwa na “taarifa za kuaminika” zinazohusisha miili iliyopatikana msituni na vifo vya “wafuasi kadhaa wasio na hatia na walio hatarini” wa Odero.

Odero na Nthenge wanashiriki “historia ya uwekezaji wa biashara” ikiwa ni pamoja na kituo cha televisheni ambacho kilitumiwa kupitisha “ujumbe mkali” kwa wafuasi, Kiprop alisema katika nyaraka za mahakama.