Kenya ilisema Alhamisi kuwa inachunguza madai kwamba maelfu ya kondomu zilizotolewa, vyandarua na dawa za kuokoa maisha ziliibwa kutoka kwa ghala la serikali na kisha kuuzwa kwenye soko kiharamu.
Bidhaa hizo zilitolewa na shirika la misaada la Global Fund lenye makao yake Geneva ambalo limetoa zaidi ya dola bilioni 1.4 kwa Kenya tangu 2003, kupambana na VVU, kifua kikuu na malaria.
Ukaguzi wa hivi majuzi wa hazina hiyo ulidai kuwa takribani kondomu milioni 1.1, vyandarua 908,000 na dawa za kifua kikuu zenye thamani ya $91,000 (euro 83,000) ziliibwa kutoka kwa Wakala wa serikali wa Kenya Medical Supplies Agency (KEMSA) na kuuzwa tena katika soko la kibiashara kwa maduka ya dawa ya kibinafsi.
“KEMSA iko katika harakati za kuchunguza madai ya Global Fund” shirika hilo lilisema, na kuongeza kuwa “mageuzi ya lazima kushughulikia masuala yaliyotambuliwa tayari yamewekwa.”
Ripoti hiyo, iliyotolewa Machi 11, inashutumu KEMSA kwa kupandisha pakubwa thamani ya dawa hadi kufikia dola milioni 5.6, ikiwa ni pamoja na kuzidisha bei ya dawa zilizoisha muda wake hadi mara 100 ya gharama halisi.
“Ghala la kuhifadhi la KEMSA la Nairobi lilikuwa limejaa bidhaa wakati wa ziara yetu, na hivyo kufanya kuwa vigumu kufuatilia bidhaa,” Global Fund ilisema, ikilaumu “udhibiti mbaya wa ndani.”
Uchunguzi sasa unaendelea, chombo hicho kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kilisema, kilisema Jumatano “Ofisi ya Inspekta Jenerali haitoi maoni yoyote kuhusu uchunguzi wowote unaoendelea hadi pale utakapokamilika na kuchapishwa.”
Ufichuzi huo unaweza kuweka ufadhili wa mfumo wa huduma ya afya nchini Kenya hatarini na unakuja wakati hospitali nchini Kenya — zimelemazwa na janga la coronavirus – tayari zinakabiliwa na uhaba wa dawa muhimu.
“Hatua ya kiutawala tayari imechukuliwa na inaendelea kuchukuliwa kwa waliohusika,” KEMSA ilisema.
Si mara ya kwanza kwa KEMSA kushutumiwa kwa ulaghai.
Mnamo 2020, ilikuwa katikati ya kashfa ya ufisadi baada ya maafisa wa serikali na wafanyabiashara kudaiwa kuiba dola milioni 400 za pesa za umma zilizotengwa kwa ajili ya vifaa vya matibabu vinavyohitajika katika vita dhidi ya Covid-19.
Kipindi cha runinga kiitwacho “Covid millionaires” kilipeperusha madai hayo kwa mara ya kwanza mnamo Agosti 2020, na kusababisha wafanyikazi kugoma katika hospitali zilizokosa vifaa muhimu nchini Kenya.
Kufuatia maandamano ya wahudumu wa afya, Rais Uhuru Kenyatta alivunja usimamizi mkuu wa KEMSA na kuamuru wizara ya afya kuchapisha maelezo ya ununuzi wote uliofanywa wakati wa janga hilo.
Licha ya taasisi ya kupambana na rushwa nchini humo kuandika ushahidi wa ufisadi, kesi zimesonga mahakamani na hakuna aliyehukumiwa hadi sasa.