Kenya yaondoa masharti ya kukabilina na UVIKO 19, ikiwemo kuvaa barakoa

Kenya ilisema Ijumaa inaondoa hitaji la watu kuvaa barakoa hadharani kama sehemu ya kupunguza masharti ya kupamban na UVIKO-19 yaliyowekwa kwa miaka miwili.

Tangazo hilo linakuja wakati viwango vya maambukizi ya UVIKO-19 katika taifa hilo la Afrika Mashariki vikiwa vimepungua hadi asilimia moja au chini zaidi katika mwezi mmoja uliopita, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema.

“Uvaaji wa lazima wa barakoa katika maeneo ya wazi ya umma sasa umeondolewa,” Kagwe alisema katika taarifa yake, huku akihimiza kuendelea kwa matumizi ya barakoa katika shughuli za ndani.

Mashabiki wa mpira na michezo mingine waliopata chanjo kamili wataruhusiwa kurudi katika kumbi za michezo na ibada zote za ana kwa ana zinaweza kuanza tena mradi tu wale wanaohudhuria wamepata chanjo, alisema.

Waziri pia alitangaza kuondolewa kwa hitaji la vipimo vya PCR kwa wasafiri walio na chanjo kamili kwenda Kenya, ingawa wageni ambao hawajachanjwa watalazimika kuchukua vipimo vya antijeni na kujitenga ikiwa wana virusi.

Jumla ya watu 5,644 wamekufa kwa Covid kati ya maambukizo 323,160 nchini Kenya tangu kisa cha kwanza kurekodiwa nchini mnamo Machi 12, 2020, kulingana na takwimu rasmi.

Kagwe alisema hatua zilizoletwa nchini Kenya tangu kuanza kwa janga hilo zimeokoa nchi kutoka kwa “janga hatari zaidi”lakini akaonya: “Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba tayari tumetoka kwenye hatari”.

Takriban asilimia 29 ya watu wazima nchini Kenya sasa wamechanjwa, kulingana na takwimu za hivi punde za serikali.