Kenya yawaachilia waendesha bodaboda 16 waliokuwa wameshikiliwa kwa kumnyanyasa kijinsia dereva mwanamke

Mahakama ya Kenya Jumatatu iliwaachilia huru waendesha bodaboda 16 waliokamatwa kwa shambulio dhidi ya mwanadiplomasia wa kike baada ya serikali kukosa kutoa ushahidi wowote dhidi yao.

Waendeshaji bodaboda hao walikusanywa mapema mwezi huu baada ya video iliyosambaa mtandaoni iliwaonyesha wanaume wakimshika nguo msichana huyo na kumpapasa huku akipiga mayowe kuomba msaada kutoka ndani ya gari, ambalo mlango wake ulikuwa umefunguliwa kwa lazima.

Mahakama ya Nairobi iliamuru waachiliwe huru mara moja baada ya upande wa mashtaka kusema hawakuwa na ushahidi wa kutosha kuwahusisha waendeshaji bodaboda hao na uhalifu.

“Kwa kuwa afisa mpelelezi hajapata ushahidi wa kuwashtaki washukiwa, ninawaachilia,” aliamuru hakimu mkuu mwandamizi Martha Nanzushi.

Mwanaume wa 17, anayedaiwa kuwa kiongozi wa shambulio hilo, hata hivyo atakabiliwa na hukumu, na anakabiliwa na kifungo cha maisha jela ikiwa atapatikana na hatia ya unyanyasaji wa kingono.

Alikamatwa wiki mbili zilizopita karibu na mpaka wa Tanzania, takriban kilomita 430 kaskazini magharibi mwa Nairobi baada ya kukwepa kukamatwa kupitia mfereji wa maji taka, polisi walisema.

Shambulio hilo lilizua ghasia nchini Kenya huku makundi ya wanawake wakifanya maandamano katika mji mkuu wa Nairobi kupinga vitendo vya waendesha bodaboda.

Rais Uhuru Kenyatta aliagiza msako mkali dhidi ya waendesha bodaboda na kuwaagiza maafisa wa sheria kuhakikisha wahusika wanaadhibiwa.

Madereva wa bodaboda nchini Kenya kwa kawaida ni vijana na wanajulikana kwa kukiuka kanuni za barabara na kuwashambulia madereva baada ya kuhusika katika ajali.

Bodaboda ni njia maarufu ya usafiri nchini Kenya, kuna angalau bodaboda milioni 1.4 zilizosajiliwa nchini Kenya, kulingana na data ya serikali ya 2018, na nyingi zinatumika kama teksi.

Waendeshaji hao mara nyingi wameshutumiwa na vikundi vya kampeni kwa wizi wa unyang’anyi na kuwanyanyasa watumiaji wengine wa barabara, unyanyasaji huo mara nyingi ukiwa ni matusi hadi ubakaji.

Mnamo 2020, kundi la waendeshaji bodaboda walijaribu kumuua mkuu wa zamani wa jeshi baada ya mmoja wao kugonga gari lake. Katika tukio jingine, gari la Naibu gavana liliteketezwa moto baada ya kuhusika katika ajali na bodaboda.

Waendesha boda-boda mwaka wa 2019 waliainishwa kama “tishio kwa usalama wa taifa” na kitengo cha utafiti cha wizara ya mambo ya ndani.