Kesi Ya Lissu Yaahirishwa Kwa Muda Usiojulikana

Kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu imeahirishwa kwa muda usiojulikana hadi pale itakapopangwa ratiba mpya ya mwendelezo wa shauri hilo.

Kesi Ya Lissu Yaahirishwa Kwa Muda Usiojulikana

Kesi hiyo leo ilikuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji kwa hatua ya kusikiliza shahidi wa nne wa upande wa Jamhuri ambapo shahidi huyo ni wa siri.

Kabla ya ahirisho upande wa Jamhuri ulimtambulisha shahidi wao ambaye ni P11 aliyefichwa katika kizimba cha siri cha shahidi ambapo si wafatiliaji wala mtuhumiwa waliomuona.

Hatua hiyo ilimfanya mshatakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo kupinga utaratibu huo akisema ni utaratibu unaokiuka tafsiri ya “kizimba maalum cha shahidi” kama ilivyoelezwa katika Kanuni ya Tatu ya Ulinzi wa Mashahidi.

Lissu alitumia hoja saba kupinga utaratibu huo akijikita katika tafsiri za kanuni za ulinzi wa mashahidi lakini pia akirejelea uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu kuhusu ulinzi wa mashahidi katika ombi lililotolewa na Jamhuri mapema wakati kesi hii inaanza, ya kwamba baadhi ya mashahidi wao watakua wa siri.

“Kwa mujibu wa kanuni hizo, kizimba maalum ni eneo ambalo shahidi haonekani na mtu yeyote isipokuwa majaji. Lakini hapa, majaji wenyewe hawawezi kumuona shahidi jambo ambalo halikubaliki kisheria,” alieleza Lissu.

Aidha, Lissu alihoji uhalali wa shahidi ambaye hata mahakama na mshtakiwa hawamfahamu, akitaka ufafanuzi wa aina ya shahidi anayelindwa kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi

“Shahidi anayelindwa ni yule aliye chini ya amri ya ulinzi inayotolewa na mahakama. Swali ni, unamlindaje mtu usiyemfahamu?” alihoji Lissu.

Katika hoja nyingine,Lissu  alieleza kuwa amri ya awali ya ulinzi wa mashahidi iliyotolewa na Mahakama Kuu ina ukomo, na hivyo inapaswa kufafanuliwa upya huku Kanuni ya 7(1) inayozungumzia ukomo wa amri za ulinzi na athari zake.

Alisisitiza kuwa ni muhimu kujua ni muda gani amri hizo zinadumu na kama bado zina nguvu kisheria katika hatua hii ya shauri.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, upande wa mashtaka wenye mawakili wanne wakiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga, ulieleza kwamba mapingamizi yaliyotolewa na mshtakiwa yanahitaji muda zaidi kujibiwa kwa kina, kwani yanagusa vifungu kadhaa vya sheria za ndani na za kimataifa.

“Mshtakiwa amewasilisha hoja nyingi za kisheria, zikiwemo rejea za kesi, mamlaka mbalimbali na tafsiri za kimataifa. Tunahitaji muda wa kutosha kuzifanyia uchambuzi wa kina,” alisema Wakili wa Serikali Mkuu Katuga.

Hata hivyo, alikumbusha kuwa kwa mujibu wa notisi chini ya kifungu cha 215, shauri hilo lilipaswa kumalizika leo, kwani ni siku ya mwisho ya vikao vya sasa vya mahakama.

Kutokana na hali hiyo, Katuga aliomba ahirisho ili wakajipange kwa ajili ya kuja kujibu hoja za mshtakiwa ambazo amezitoa.

Baada ya kusikiliza hoja hizo jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, walikubaliana na hoja ya ahirisho huku akieleza kuwa kesi hiyo itaendelea mara tu ofisi ya Msajili itakapotoa ratiba nyingine ya mwenendo wa kesi ambapo haijajulikana ni lini ratiba hiyo itatolewa hivyo itakapotolewa pande zote zitajulishwa.

Itakumbukwa kuwa kesi hiyo ilianza kusikilizwa rasmi Septemba 28, 2025 ambapo ilianza kwa mapingamizi hadi leo Novemba 12, 2025 ambapo kwa mujibu wa ratiba ya mtiririko wa kesi inafika ukomo leo ambapo ratiba hiyo ilionyesha kwamba ndio siku ya hukumu.

Hata hivyo kwa kuwa  kesi hiyo haikwenda kama ratiba ilivyopangwa kwa maana bado ushahidi haujamalizika  basi itaendelea pindi ratiba mpya utakapotolewa.

Lissu ambaye mbali na kuwa kiongozi mkuu wa chama cha upinzani Tanzania pia ni Mwanaharakati na Mwanasheria mashuhuri nchini humo, anakabiliwa na mashtaka ya Uhaini anayodaiwa kuyafanya kupitia hotuba yake kwa wanahabari aliyoitoa Aprili 3, 2025.

Alikamatwa mkoani Ruvuma kwa mara ya kwanza Aprili 9, 2025 na kufikishwa Mahakama ya Kisutu Aprili 10, 2025.

Leo anatimiza Siku 224 gerezani kutokana na kesi hiyo kutokua na dhamana.