Ndoto ya kiongozi wa chama cha Republican katika bunge la Congress, Kevin McCarthy kuwa spika wa bunge hilo la Marekani lilizimwa kwa mara ya 11 katika siku ya tatu ya upiga kura.
Sasa kinachosubiriwa kuona iwapo hatimaye atafanikiwa kuwa kuongozi wa bunge hilo au la.
Kundi la wabunge 20 wenye msimamo mkali wa chama chake cha Republican wameapa kupigana kwa jino na ukucha kuhakikisha Bw McCarthy anakosa kura 218 zinazohitijaka kumpa wadhifa huo wa uspika wa bunge hilo.
Chama cha Republicana kilichukua uongozi wa bunge la Congress katika uchaguzi wa katikati mwa muhula mwezi novemba mwaka wa 2022, lakini utata huo umelemaza zoezi la kuwaapisha wabunge kwani spika anapaswa kuchaguliwa kabla yao kuapishwa.
Bunge hilo lilikuwa limehairishwa hadi ijumaa ya leo ambapo litakuwa linarejelea kikao chake na kuendelea mchakato wa kutafuta spika mpya.
Mwaka wa 1860, wakati Marekani ulipokuwa ukivutana kuhusu suala la utumwa ndipo bunge lilipiga kura mara nyingi kuchagua spika. Wakati huo ikichukua duru 44 za kura kupata spika.
Lakini chanzo cha McCarthy kukataliwa mara si haba ni nini haswa? Kundi la wabunge 20 wa chama cha Republican wamedinda kumpa ridhaa ya kuwa spika kwa misingi kuwa hawamwamini yeye wala sera zake.
Waasi hao wana mashaka na mbunge huyo wa California, licha yake kuidhinishwa na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.
Mmoja wa wapinzani, Ralph Norman wa Carolina Kaskazini anashikilia kuwa hana imani na bwa McCarthy au hata falsafa zake.
Mbunge huyo alisema upande wa McCarthy ilitishia kulipiza kisasi cha kisiasa dhidi yao ikiwa hawangejiunga nao wiki chache kabla ya shughuli hiyo.
“Tulikuwa tunaenda kutupwa nje ya kamati, tutapoteza kila fursa tuliyokuwa nayo,” alisema bw Norman.
Wakati huohuo, Wademokrat walio wachache waliendelea kumpigia kura kwa pamoja kiongozi wao Hakeem Jeffries wa New York ambaye ndiye mtu wa kwanza mweusi kuwahi kuongoza chama katika Bunge la Congress.
Lakini inaonekana hakuna uwezekano kwamba anaweza kushindwa zaidi ya wanachama sita wa Republicana kuwa spika.
Wabunge katika bunge lililogawanyika vikali watakutana tena leo Ijumaa, siku ya kumbukumbu ya pili ya ghasia za wafuasi wa Trump katika ikulu ya Marekani.