Kikundi cha densi cha Uganda, Ghetto Kids kimeshindwa kufika fainali ya Britain’s Got Talent

Kikundi cha densi cha Uganda Ghetto Kids

Kikundi cha densi cha Uganda Ghetto Kids kilikosa nafasi tatu za juu katika hatua ya mwisho ya shindano la Britain’s Got Talent siku ya Jumapili, na kuwashukuru mashabiki kwa “uungwaji mkono wao usioyumba wakati wote wa shindano hilo”.

Kundi hilo la watoto sita wana umri wa kati ya miaka sita na 13, na walitoka katika jamii maskini katika mji mkuu wa Uganda Kampala kabla ya kuchukuliwa na kulelewa na mlezi wao aliyegeuka meneja Dauda Kavuma.

Ghetto Kids ilikuwa miongoni mwa waliofika fainali 10 katika shindano hilo – ambalo lilishindwa na Viggo Venn, mcheshi mwenye umri wa miaka 33 kutoka Norway.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na mchezaji densi Lilliana Clifton mwenye umri wa miaka 13 huku Cillian O’Connor, 14, akiibuka wa tatu.
Kundi hilo la Uganda tayari limeweka historia baada ya kuwa wasanii wa kwanza kupewa “golden buzzer” na mmoja wa majaji kabla hata hawajamaliza uchezaji wao – jambo ambalo liliwapeleka moja kwa moja nusu fainali.

Kisha walipata kura nyingi zaidi za umma, na kuwapa nafasi kwenye fainali pamoja na washiriki wengine tisa.

Imeongeza umaarufu mkubwa wa kikundi hicho – Ghetto Kids tayari ilikuwa na mamilioni ya maoni kwenye chaneli yao ya YouTube kabla ya kujiunga na onyesho hilo la vipaji la Uingereza, na ilionyeshwa kwenye video ya muziki ya mwimbaji nyota wa rap wa Marekani-Morocca French Montana mwaka wa 2017.