Kimbunga chawaua watu wanane nchini Msumbiji


Kimbunga kiligonga kaskazini mwa Msumbiji na kusababisha vifo vya takriban watu wanane siku ya Ijumaa, taasisi ya kitaifa ya kudhibiti hatari ilisema.

Miongoni mwa waathiriwa ni mtoto aliyepondwa katika nyumba iliyoporomoka huko Monapo, taasisi hiyo ilisema, na kuongeza idadi ya watu waliokufa hadi wanane.
Rais Filipe Nyusi alikuwa ametangaza mapema katika ziara yake nchini Afrika Kusini kwamba watu saba wamefariki.

Kimbunga Gombe kilipiga mkoa wa Nampula usiku wa Alhamisi-Ijumaa kikiambatana na upepo mkali — kilitabiriwa kufikia kilomita 160 kwa saa (100 mph) — na mvua, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa nyumba, huduma ya hali ya hewa ilisema.

“Taarifa za awali zinaonyesha kuwa watu saba walifariki, wawili katika jiji la Nampula kutokana na kuporomoka kwa nyumba na watano mjini Angonche,” kilomita 170 kuelekea kusini mashariki mwa Bahari ya Hindi, rais alisema alipokuwa Pretoria.

“Kuna matatizo ya mawasiliano na wilaya zilizoathirika zaidi zikiwa za huko Nampula,”aliongeza, akionya juu ya hatari ya mafuriko kutoka Mto Licungo.
“Kuna miti minga nguzo za umeme zilizoanguka na zinaweza kusababisha madhara,” Nyusi alisema.

Kimbunga hicho kilidhoofika hadi dhoruba ya kitropiki baadaye Ijumaa lakini mvua kubwa iliendelea kunyesha katika mikoa jirani.
Umeme na maji vilikatika mjini Nampula ambapo huduma ya simu za mkononi ilitatizika, ripoti zilisema.

Safari za ndege kuelekea jimboni humo zilikuwa zimesitishwa kabla ya kimbunga hicho kutokea, shirika la ndege la kitaifa LAM lilisema.
Makundi ya misaada yalikuwa yanajiandaa kutumwa katika eneo hilo baada ya Dhoruba ya Tropiki Ana mnamo Januari kuacha uharibifu na kuua takriban watu 100 kote Madagascar, Msumbiji, Malawi na Zimbabwe.