Search
Close this search box.
Africa

Kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso atangazwa kuwa rais

14
Rais mpya wa Burkina Faso Paul-Henri Sandaogo Damiba AFP PHOTO /Radiodiffusion Télévision du Burkina”

Mwanajeshi aliyeongoza mapinduzi Burkina Faso, Paul-Henri Sandaogo Damiba, ametangazwa kuwa rais na baraza kuu la kikatiba la nchi hiyo baada ya mapinduzi mwezi uliopita, vyanzo vya kisheria vilisema Alhamisi.

Baraza la Kikatiba Jumatano liliamua kwamba “Paul-Henri Sandaogo Damiba, Luteni Kanali katika Vikosi vya Wanajeshi vya Kitaifa, rais wa Patriotic Movement for Preservation and Restoration (jina rasmi la jeshi hilo), ndiye rais” wa Burkina Faso.

Damiba pia ni mkuu wa nchi na kamanda mkuu wa vikosi vya jeshi.

Hatua hiyo ilithibitisha tangazo la jeshi mnamo Januari 31 kwamba Damiba atateuliwa katika majukumu hayo kwa kipindi cha mpito, na atasaidiwa na makamu wawili wa rais.

Katika taarifa iliyotolewa baadaye Alhamisi, Baraza la Katiba lilisema kuwa kuapishwa rasmi kwa Damiba kutafanyika Februari 16 katika mji mkuu wa Ouagadougou.

Mnamo Januari 24, maafisa wasioridhika wakiongozwa na Damiba walimuondoa uongozini Roch Marc Christian Kabore, ambaye alikuwa amekabiliwa na wimbi la hasira ya umma kutokana na jinsi alivyoshughulikia uasi wa kijihadi uliosababisha maafa ya wengi.

Ikikabiliwa na shinikizo kutoka kwa washirika wa Burkina Faso katika Afrika Magharibi, mahakama ya kijeshi wiki iliyopita ilibatilisha kusimamishwa kwa katiba na kufuta amri ya kutotoka nje usiku kucha.

Lakini suala kuu la tarehe ya uchaguzi bado halijatatuliwa.

Mnamo Januari 24, jeshi iliapa kurejesha uongozi wa katiba ndani kwa wakati unaofaa.

Siku ya Jumamosi, ilitangaza kuwa tume ya wanachama 15 itaundwa kwa lengo la “kutayarisha rasimu ya katiba na ajenda, pamoja na pendekezo la muda wa kipindi cha mpito.”

Jopo hilo litapewa wiki mbili kuripoti matokeo.

Ikiwa  moja ya nchi maskini zaidi duniani, Burkina Faso inapambana na wanajihadi ambao wamesababisha vifo vya zaidi ya 2,000 na kuwalazimu karibu milioni 1.5 kukimbia makazi yao.

Nchi hiyo imesimamishwa kutoka uanachama wa jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS, ingawa iliepuka vikwazo kufuatia kurejeshwa kwa katiba wiki iliyopita.

Siku ya Jumatano, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilionyesha “wasiwasi mkubwa” juu ya “mabadiliko ya serikali kinyume na katiba” ya Burkina Faso, lakini likachagua kutoyaelezea kama mapinduzi ya kijeshi au hata kuyashutumu moja kwa moja.

Comments are closed

Related Posts