Kiongozi wa kijeshi wa Mali Assimi Goita amesema kwamba yuko tayari kufanya mazungumzo na jumuiya ya kikanda ya ECOWAS baada ya taifa hilo kuwekewa vikwazo kutokana na kucheleweshwa kwa uchaguzi.
“Hata kama tunajutia uamuzi wa ECOWAS usio halali, ulio haramu na usio wa kibinadamu ya baadhi ya maamuzi yaliyochukuliwa, Mali ipo tayari kwa mazungumzo na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ili kupata muafaka,” Goita alisema kwenye TV ya serikali baada ya umoja huo kuweka vikwazo vya biashara na kizuizi cha mpaka.
Viongozi wa ECOWAS pia walikubali kukata misaada ya kifedha, kufungia mali ya nchi hiyo katika Benki Kuu ya Mataifa ya Afrika Magharibi, na kuwarudisha mabalozi wao kutoka nchi hiyo.
Vikwazo hivyo vilifuatia pendekezo la serikali inayoongozwa na jeshi la Mali mwezi uliopita la kusalia madarakani kwa hadi miaka mitano kabla ya kuandaa uchaguzi — licha ya matakwa ya kimataifa kwamba iheshimu ahadi ya kufanya uchaguzi mwezi Februari.
ECOWAS pia ilikataa pendekezo lililorekebishwa la serikali lililowasilishwa kwa umoja huo usiku wa kuamkia mkutano wa kilele.
Baada ya wimbi la awali la vikwazo kutoka kwa ECOWAS kufuatia mapinduzi ya 2020, Goita alikuwa ameahidi kurejesha utawala wa kiraia Februari 2022 baada ya uchaguzi wa rais na wabunge.