Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Kiongozi wa ODM Raila Odinga aanza ziara Uingereza - Mwanzo TV

Kiongozi wa ODM Raila Odinga aanza ziara Uingereza

Raila Odinga, Kiongozi wa ODM na waziri Mkuu wa Zamani, Kenya

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga amechukua pumziko kutoka kwa kampeni za kisiasa na kuenda katika ziara ya kikazi nchini Uingereza kuanzia leo Jumatatu 14.

Katibu wa habari katika sekretarieti ya kampeni ya urais ya Raila Odinga 2022, Dennis Onsarigo alithibitisha kwamba Bw Odinga aliondoka nchi siku ya Jumapili usiku katika ziara itakayomkutanisha na maafisa wakuu wa serikali ya Uingereza, kufanya mazungumzo na kukutana na Wakenya wanaoishi Uingereza.

Timu yake ya kwanza, iliondoka Jumamosi muda mfupi baada ya mkutano wa hadhara wa Jacaranda Grounds uliofanyika siku ya Jumamosi.

 Raila Odinga atakuwa anaongoza wajumbe wanaojumuisha aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, Magavana Hassan Joho (Mombasa), Charity Ngilu (Kitui), Lee Kinyanjui (Nakuru) na Wycliffe Oparanya (Kakamega), Seneta wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed na Ben Agina ambaye ni mshauri wa Bw Odinga kuhusu masuala ya kimataifa na ushiriki wa diaspora.

Kulingana na ratiba ya Bw Odinga atakutana na Waziri wa Majeshi wa Uingereza James Heappey.
Kuna mahojiano na vyombo vya habari yaliyopangwa siku moja kabla ya mkutano na mjumbe wa kibiashara wa Waziri Mkuu wa Uingereza nchini Kenya Theo Clarke mjini Westminster.

Siku ya Jumatano, Bw Odinga atakutana na Lord Tarif Ahmad, Waziri wa Uingereza wa Asia Kusini, Afrika Kaskazini, Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola katika Ofisi ya Kigeni, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO).
Pia atatoa hotuba katika Kituo cha ThinkTank cha Chatham House.

Baadaye jioni, atakuwa kwenye Uwanja wa Emirates kutazama mechi ya soka kati ya Arsenal FC na Liverpool, kwa mujibu wa ratiba rasmi.

Kisha Bw Odinga atakutana na Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby siku ya Alhamisi katika Jumba la Lambeth, ambalo ni makazi yake rasmi.
Siku hiyo hiyo, atakutana na Wakenya wanaoishi Uingereza.

Safari ya Bw Odinga kuenda Uingereza inafuatia ile ya Naibu Rais William Ruto hivi majuzi.
Naibu Rais William Ruto pia alikutana na viongozi wa serikali, Askofu Mkuu wa Canterbury na kutoa hotuba katika Chatham House.

Atakaporejea nchini, Bw Odinga atakuwa anarudi kwenye kampeini hii ikijumuisha kuzindua Brigedi ya Vijana na Raila.