Kirusi kipya cha Corona, Omicron chazua wasiwasi kote duniani

Takriban miaka miwili baada ya kulipuka kwa janga la UVIKO-19, ulimwengu unakabilina na kirusi kipya cha corona ambacho kinaweza kuwa hatari zaidi kuliko kile kilichochea mawimbi ya maambukizi katika mabara tofauti duniani.

Jopo la Shirika la Afya Duniani lilikipa kirusi hicho jina  “Omicron” na kukiainisha katika kitengo kimoja na kirusi kinachoambukiza kwa kasi cha delta, ambacho bado kinasababisha visa vipya vya ugonjwa huo na vifo barani Uropa na Amerika.

 “Kirusi hicho kinaonekana kuenea kwa haraka,” Rais wa Amerika Joe Biden alisema Ijumaa kuhusu kirusi hicho kipya, siku moja tu baada ya Waamerika kusherehekea sikukuu ya Thankgiving huku wengi wakitarajia kurudi kwa maisha ya kawaida hususan kwa wale waliochanjwa.

 Huku akitangaza vizuizi vipya vya usafiri, Biden aliwaambia waandishi wa habari, “Nimeamua kuwa tutakuwa waangalifu.”

Kiwango cha hatari halisi ya kirusi cha Omicron bado hakijaeleweka,lakini utafiti wa awali unaonyesha kuwa kina uwezo wa kuambukiza mtu mmoja mara kadhaa ikilinganishwa na aina nyingine zinazoambukiza kwa haraka, WHO ilisema. Hiyo inamaanisha kuwa watu walioambukizwa UVIKO 19 na kupona wanaweza kuambukizwa tena. Itauchukua muda wa wiki ili kujua kama chanjo za sasa zitafaulu kudhibiti kirusi hicho.

Shirika la Afya Duniani WHO

Kutokana na kugunduliwa kwa kirusi hicho katika mataifa ya kusini mwa Afrika, Amerika, Canada, Urusi na mataifa mengine mengi yalijiunga na Umoja wa Ulaya katika kuwawekea marufuku wasafiri kutoka eneo hilo, ambapo kirusi hicho kimechangia ongezeko jipya la maambukizi.

Ikulu ya White House ilisema Amerika itawawekea marufuku wasafiri kutoka Afrika Kusini na nchi nyingine saba kutoka eneo hilo kuanzia Jumatatu. Biden alitoa tangazo hilo Ijumaa na kusema kuwa raia wa Amerika na familia zao wataruhusiwa kuingia nchini.

Wataalamu wa matibabu, ikiwa ni pamoja na WHO, walionya dhidi ya kueneza wasiwasi kuhusu kirusi hicho kabla hakijachunguzwa kwa kina. Ila wasiwasi umeenea zaidi baada ya janga la UVIKO 19 kusababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 5 kote duniani.

Kirusi cha Omicron sasa kimetambuliwa kwenye wasafiri kutoka Ubelgiji, Hong Kong na Israel, na pia kusini mwa Afrika.

Hakukuwa na dalili kuonyesha iwapo kirusi hicho kinasababisha madhara zaidi kama ilivyo na virusi vingine, watu wengine walioambukizwa hawaonyeshi dalili zozote, wataalam wa Afrika Kusini walisema. Jopo la WHO lilitoa jina Omicron kutoka kwa alfabeti ya Kigiriki kama ilivyofanya na virusi vya awali.

Uingereza, nchi za EU na zingine ziliweka vizuizi  vya usafiri Ijumaa, mataifa mengine yaliweka marufuku ndani ya saa chache baada ya kugunduliwa kwa kirusi hicho.

Biden alipoulizwa kwa nini Amerika itaweka vizuizi kutoka Jumatatu, Biden alisema “Kwa sababu hilo lilikuwa pendekezo lililotoka kwa timu yangu ya matibabu.