Kizza Besigye: Uongozi sharti urejeshwe kwa wananchi wa Uganda

Kiongozi wa zamani wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye.

Kiongozi wa zamani wa upinzani na mwanaharakati mkuu nchini Uganda Kizza Besigye, amedokeza kuwa yeye pamoja na wanaharakati wengine watapigania hadi mwisho kukomesha utawala wa kiimla kwa kumiliki silaha ambao umelemaza maendeleo na ukuaji wa taifa hilo.

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na Mwanzo TV, kiongozi huyo wa zamani wa upinzani amebainisha kuwa anatetea mabadiliko ya mamlaka katika taifa hilo ambayo yamechelewa kwa muda mrefu.

“Kwetu sisi uhamasishaji wetu wa nchi ni kurudisha madaraka kwa wananchi. Uganda inahitaji mpito, sio urithi kwa kuwa wamekuwa wakijaribu kuwachanganya watu kwamba tunahitaji kizazi kipya ambacho Muhoozi anawakilisha,” alisema Besigye.

Besigye amesisitiza kwamba uongozi nchini Uganda unatekelezwa kupitia jeshi ambalo alibaini kuwa linawafahamisha raia kuhusu mfalme wa kifalme anayekuja.

“Mapambano ni kuhamisha udhibiti wa mamlaka kutoka kwa watu wenye silaha hadi kwa watu sio kutoka kwa wazee hadi kwa vijana. Mtu yeyote anayewakilisha utawala wa bunduki tunamtaka aangushwe. Na hapo ndipo tutakuwa na mabdiliko ya kweli ya mamlaka bila kutumia bunduki.” amesisitiza Besigye.

Aidha Besigye amewaonya wakenya dhidi ya kupuuza mjadala wa kuondoa mihula ya urais akisema unaweza kuwa mwanzo wa utawala wa kidikteta jinsi ilivyo nchini Uganda.

“Ushauri wangu ungekuwa kwamba hakuna kitu kama hicho kichukuliwe kirahisi na kusema ukweli tunachukulia Kenya bado iko kwenye kipindi cha mpito, demokrasia haijaunganishwa. Mafanikio muhimu ambayo Kenya imepata yanaweza kurejeshwa nyuma na mawazo ambayo yameanza,” amesema Besigye.

Dkt Besigye wakati huohuo amewataka wakenya kuwa waangalifu kuhusu kile mwana wa kiume wa rais wa Uganda Yoweri Museveni Jenerali Muhoozi Kainerugaba alichokuwa anatuma kwenye mitandao kuhusu Kenya pamoja na mkono wa Kampala katika mzozo unaoendelea mashariki mwa DR Congo ambapo Kenya ilituma wanajeshi wake hivi majuzi.

Kiongozi huyo amesema kupandishwa cheo kwa Muhoozi kuwa jenerali ni kumuandaa kwa ajili ya kurithi mikoba ya uongozi wa nchi ya Uganda kutoka kwa babake Yoweri Museveni.

Wiki mbili tu baada ya kutoa matamshi tatanishi yalioashiria kuwa ingemchua wiki mbili tu kuteka Nairobi iwapo Uganda ingeivamia Kenya, Muhoozi alipandishwa cheo kutoka nafasi ya awali kama mkuu wa kitengo cha nchi kavu cha Jeshi la ulinzi la wananchi wa Uganda.

“Madaraka yanapatanishwa kupitia jeshi na familia yake. Ndio maana Muhoozi amekuwa katika uongozi wa kijeshi kwa sababu huko ndiko kunakohitajika urithi. Urithi upo jeshini kwa sababu Museveni mwenyewe yuko jeshini,” alisema Besigye.

https://www.youtube.com/watch?v=NwAaC0KZne4