Korea Kusini: Mgombea urais aahidi bima ya afya kwa wanaume wanaopoteza nywele

Watu waliopoteza nywele nchini Korea Kusini wanapaswa kushughulikiwa matibabu yao na serikali ili kuzuia “ubaguzi” mgombea urais wa chama tawala aliahidi Ijumaa, katika kile wakosoaji walichokiita njia yake ya kupata umaarufu nchini humo kabla kufanyika kwa uchaguzi.

Mgombea wa Chama cha Demokrasia Lee Jae-myung alisema atapanua bima ya afya ya serikali ili kugharamia matibabu, ambayo yanaweza kujumuisha upandikizaji wa nywele ghali, ikiwa atashinda katika uchaguzi wa urais wa mwezi Machi.

“Nitapanua bima ya afya kwa wote ili watu wenye upara wapate dawa za matibabu … na pia nitazingatia kupatikana kwa bima ya afya itakayosaidia upandikizaji wa nywele kwa watu wenye tatizo sugu la upotezaji wa nywele,” alisema kwenye mtandao wa Facebook.

Lee, mwanasheria wa haki za binadamu aliyegeuka kuwa mwanasiasa, alisema watu wenye matatizo ya kupoteza nywele wamekabiliwa na ubaguzi kwa muda mrefu.

Katika video fupi iliyochapishwa mtandaoni Ijumaa, Lee, ambaye haonekani kuwa na tatizo la upotezaji wa nywele, anaonekana akiaahidi kila mtu kuwa na nywele nzuri zilizojaa kichwani kama yeye.

Wakorea wengi wanatumia dawa zisizo na tija na zinazoweza kusababisha madhara zaidi. Matibabu ya upotezaji wa nywele kwa sasa hayajumuishwi katika bima, Lee alisema, akielezea ahadi yake mpya ya kampeni.

Suala hilo linaathiri raia mmoja kati ya watano wa Korea Kusini, kampeni yake ilisema, bila kutoa maelezo kuhusu kiasi gani inatarajiwa kutumiwa katika kutimiza ahadi hiyo.

Ahadi hiyo – ambayo ilitolewa mara ya kwanza wiki jana — imezua mjadala mkubwa wa umma, huku wapiga kura wengi wakijitokeza kuunga mkono.

“Kupoteza nywele ni ugonjwa. Ninaidhinisha ahadi yake kikamilifu,”mfuasi mmoja aliandika kwenye Daum, tovuti ya mtandaoni ya pili kwa ukubwa nchini humo.

Lakini wakosoaji wengine wamekashifu hatua hiyo wakisema bima hiyo itapunguza bima ya afya kwa magonjwa mengine ambayo ni hatari zaidi.

Lee ni mmoja wa wagombea wawili wanaoongoza katika uchaguzi wa rais Korea Kusini.

Yupo katika kinyang’anyiro kikali na mgombea wa upinzani Yoon Suk-yeol.

Rais wa sasa Moon Jae-in amezuiliwa kisheria kuwania muhula wa pili na ameratibiwa kuondoka uongozini mwezi Mei.