Mafuta na ushuru vimetajwa kuwa vipengele vinavyosababisha gharama ya juu ya umeme, jopo la Seneti limeambiwa.
Ufichuzi huo uliibuka wakati wa uchunguzi kuhusu chanzo cha gharama ya juu ya umeme na kamati inayoongozwa na Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga mnamo Jumanne.
Kamati ya Seneti ya Kawi iliwapa kazi maafisa wa usimamizi wa Rabai Power kueleza ni kwa nini wanazalisha nguvu kidogo lakini wanavuna faida kubwa.
Jopo hilo lilishangazwa na jinsi mtambo wa kuzalisha umeme unavyovuna Sh7.36 bilioni kila mwaka kwa kuzalisha megawati 90 pekee za nishati hiyo.
Meneja Mkuu wa Rabai Power Zablon Okwoku alisema kuwa mtambo huo unaoendeshwa na Heavy Fuel Oils (HFO) ni kipengele ambacho kinaongeza kwa kiasi kikubwa gharama za umeme kwa mtumiaji.
“Kipengele kinachochukua sehemu kubwa ya gharama ya kilowati ni sehemu ya mafuta. Iko nje ya uwezo wa jenereta,” Okwoku alisema.
“Gharama inazingatia gharama za kutua. Ushuru huchukua karibu asilimia 45 ya gharama ya operesheni. Ni bei nzuri.”
Alifichua kuwa kituo hicho kilitia saini kandarasi na Kenya Power kuzalisha umeme kwa miaka 20.