LHRC yasikitishwa na hatua ya TCRA kufungua mashtaka dhidi ya Jambo TV

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia Kamati yake ya Maudhui imefungua mashtaka dhidi ya Jambo Online TV, ikidai kuwa kituo hicho cha habari kimekiuka Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kuhusu Maudhui ya Mtandaoni za mwaka 2020, zilizofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Hatua hii inatokana na matangazo ya maudhui yaliyotajwa kuwa natuhuma nzito yaliyotolewa na kituo hicho bila kuwapa nafasi wahusika kutoa ufafanuzi wao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 9 Oktoba 2024, Mamlaka ya Mawasiliano kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, inadai kuwa tarehe 1 Oktoba 2024, Jambo Online TV inadaiwa kurusha hotuba ya Mheshimiwa Tundu Lissu, ambayo iliibua tuhuma dhidi ya viongozi wa serikali na kampuni ya Tigo.

Hotuba hiyo, ambayo ilichapishwa mtandaoni, iliweka wazi madai mazito yaliyohusisha kampuni ya mawasiliano ya simu ya Tigo, ambapo Tundu Lissu alieleza kuwa Tigo ilihusika katika njama za kumfuatilia kabla ya kushambuliwa.

Katika hotuba yake, Lissu alinukuliwa akisema, “Tigo walikuwa wakinifuatilia sio kwa njia ya kawaida tu, bali walitumia wachunguzi wa ndani kunifanyia ufuatiliaji wa kina. Mtu mmoja aliyekuwa mfanyakazi wa Metropolitan Police ya London ndiye alikuwa mchunguzi wao wa ndani, akichunguza matendo ya wafanyakazi wa Tigo. Siku tano baada ya mimi kushambuliwa, mchunguzi huyo alisikika akisema kuwa walikuwa wanajua taarifa zangu zote, hata mahali nilipokuwa.”

TCRA imeendelea kudai kuwa, siku iliyofuata tarehe 2 Oktoba 2024, Jambo Online TV ilirusha hotuba nyingine ya Bw. Erick Kabendera, mwandishi wa habari, ambapo naye alitoa tuhuma kali dhidi ya kampuni ya mawasiliano ya Vodacom. Kabendera alidai kuwa Vodacom ilihusika na mpango wa kumteka.

Katika hotuba hiyo, Kabendera alisema: “Baada ya uchunguzi wa miaka mitatu, mimi na wanasheria wangu tumekusanya ushahidi unaoonyesha wazi kwamba kampuni ya Vodacom Tanzania ilihusika katika njama za kutaka kuniteka. Kama si hatua za haraka zilizochukuliwa na mitandao ya kijamii kufichua njama hizo, pengine ningetekwa au hata kuuawa. Ushahidi huu ni mzito na unatosha kabisa kufungua mashtaka dhidi ya Vodacom hapa Tanzania na hata tanzu zake zilizoko Afrika Kusini na Uingereza.”

 

Kwa mujibu wa TCRA, Jambo Online TV inatuhumiwa kwa kukiuka Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni kwa kurusha maudhui haya bila kutoa nafasi kwa kampuni husika, pamoja na viongozi wa serikali, kutoa ufafanuzi au kujitetea. TCRA imesema kuwa hatua hii si tu imekiuka maadili ya uandishi wa habari, bali pia imeharibu sifa za taasisi za umma na kampuni za kibinafsi.

Kwa mujibu wa kanuni za TCRA, kitendo cha Jambo Online TV kueneza maudhui ya namna hii kinakiuka Kanuni ya 9 (a), inayosema kuwa mtoa huduma wa maudhui mtandaoni lazima kuhakikisha maudhui yanayotangazwa ni salama na hayavunji sheria yoyote ya nchi. Aidha, kanuni za maudhui mtandaoni zinawataka watoa huduma kuhakikisha maudhui yao yanazingatia viwango vya kitaaluma vya uandishi wa habari na kuwapa wahusika fursa ya kutoa maoni yao pale wanapotuhumiwa.

Kamati ya Maudhui ya TCRA imeitisha kikao na uongozi wa Jambo Online TV tarehe 17 Oktoba 2024 katika makao makuu ya TCRA jijini Dar es Salaam ili kutoa utetezi wao kwa tuhuma hizo. Katika barua hiyo, TCRA imeonya kuwa iwapo Jambo Online TV itashindwa kufika katika kikao hicho, hatua kali za kisheria na kiudhibiti zitachukuliwa dhidi yake.

“Kamati ya Maudhui inakitaka Kituo cha Jambo Online TV kuwasilisha utetezi rva maandishi na kufika mbele ya Kamati kujieleza kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yake kwa kukiuka Kanuni za Maudhui Mtandaoni, 2020 kama zilivyofanyiwa Marekebisho Mwaka 2022”, imeeleza taarifa