Lissu Ahitimisha Utetezi Baada Ya Siku Tano Mahakamani, Shahidi Mwingine Kuendelea

Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, leo amehitimisha kutoa ushahidi na utetezi wake katika Mahakama Kuu, baada ya kutumia siku tano akijitetea katika kesi inayomkabili.

Lissu Ahitimisha Utetezi Baada Ya Siku Tano Mahakamani, Shahidi Mwingine Kuendelea

Lissu, ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi, amehitimisha ushahidi wake kwa kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya majibu aliyoyatoa wakati akihojiwa na upande wa Jamhuri, akiwemo Wakili wa Serikali, Katuga.

Katika maelezo yake ya mwisho, Lissu amesema aliulizwa kama ni kweli au si kweli kwamba nia ya kutenda kosa inathibitishwa na matendo yenyewe, ambapo alijibu kuwa si kweli.

“Waheshimiwa Majaji, nimeulizwa swali la mwisho kwamba ni kweli au si kweli kwamba nia ya kutenda kosa inathibitishwa na matendo yenyewe, nikajibu si kweli,” amesema Lissu.

Amefafanua kuwa si makosa yote ambayo nia ya kutenda kosa inaweza kuthibitishwa kupitia matendo, akisema kuna makosa ambayo yanaweza kuthibitishwa kwa njia nyingine.

“Ufafanuzi wangu ni kwamba sio makosa yote ambayo nia inathibitishwa kwa matendo. Kuna makosa mengine yanathibitishwa kwa uchapishaji na mengine yanathibitishwa kwa matendo,” amesema.

Lissu pia amerejea suala la tuzo aliyowahi kupewa, ambalo aliulizwa na Wakili Katuga kama aliliwasilisha mahakamani kama sehemu ya ushahidi wake. Amesema hakufanya hivyo kwa sababu tuzo hiyo haikuwa sehemu ya kesi.

“Niliulizwa hapa na Wakili Katuga kuhusiana na ushahidi wangu kuhusu tuzo na niliulizwa kama niliileta hapa mahakamani, nikasema kwamba sijaleta kwa sababu sio sehemu ya kesi. Nikaulizwa ni sheria gani inayoruhusu kuleta maneno matupu,” amesema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu jibu hilo, Lissu amesema alichokuwa akieleza ni kanuni ya msingi katika sheria ya ushahidi kwenye kesi za jinai, kwamba mshtakiwa halazimiki kuthibitisha kuwa hana hatia, bali mzigo wa kuthibitisha mashtaka upo upande wa Jamhuri.

“Waheshimiwa Majaji, niliposema nilikuwa na maana kwamba kanuni kuu ya sheria ya ushahidi inasema kwamba kwenye kesi ya jinai mshtakiwa halazimiki kuthibitisha kwamba hana hatia, bali mzigo wa kuthibitisha mashtaka upo upande wa mashtaka, ndio wanatakiwa kuthibitisha hatia,” amesema.Lissu amefafanua pia majibu yake kuhusu njia za kupinga sheria anayoamini kuwa inapingana na Katiba.

Amesema alieleza mahakamani kuwa kuna njia za kimahakama na zisizo za kimahakama, ikiwemo maandamano ya kidemokrasia, na alipoulizwa ni kifungu gani kinachotambua njia hiyo, alitaja Ibara ya 20(1) ya Katiba.“Niliulizwa vilevile kwamba kwenye ushahidi kuhusu njia ya kupinga sheria zinazopingana na Katiba, nikasema njia zipo nyingi.

Kuna njia za kimahakama na kuna njia zisizokuwa za kimahakama, kwa mfano za maandamano ya kidemokrasia, na nikaulizwa ipo kwenye kifungu gani, nikajibu hiyo ipo kwenye kifungu cha 20(1),” amesema.

Ameongeza kuwa alichomaanisha ni kwamba njia hizo za nje ya Mahakama zinatambuliwa na Katiba na kwamba Mahakama imewahi kuthibitisha utambuzi huo.

Lissu pia amerejea majibu yake kuhusu mihimili mitatu ya dola. Amesema aliulizwa kuitaja na akataja Serikali, Bunge na Mahakama. Alipoulizwa kuhusu majukumu yake, alisema moja ya majukumu ya Bunge ni kutunga sheria na moja ya majukumu ya Serikali ni kusimamia sheria.

Hata hivyo, amesema majibu hayo hayakuwa na maana kwamba hayo ndiyo majukumu pekee ya mihimili hiyo.

“Waheshimiwa Majaji, niliposema moja ya kazi ya Bunge ni kutunga sheria nilikuwa namaanisha kwamba jukumu la Bunge sio kazi pekee na nilisema moja ya majukumu ya Serikali ni kusimamia sheria lakini sio jukumu moja tu la kazi ya Serikali,” amesema.

Katika sehemu nyingine ya ufafanuzi wake, Lissu amezungumzia suala la baadhi ya mashahidi waliotajwa katika kesi hiyo ambao, kwa mujibu wa maelezo yake, walikamatwa kwa tuhuma za kufanya uhalifu na baadaye kuitwa kutoa ushahidi baada ya kupewa ofa ya kufutiwa kesi zilizokuwa zinawakabili.

“Niliulizwa vilevile kuhusiana na suala la mashahidi ambao walikamatwa kwa uhalifu halafu wakaitwa Mahakamani kwa ofa kwamba wawe mashahidi, watafutiwa kesi,” amesema.

Lissu amesema hoja yake ilikuwa kwamba watu hao walikiri kufanya uhalifu na hivyo alikuwa akizungumzia uhalali na uzito wa ushahidi wao katika mazingira hayo.

“Ufafanuzi wangu ni, wamekiri kwamba walifanya uhalifu, ushahidi wangu ni kwamba hawa wahalifu…” amesema Lissu kabla ya kuendelea na maelezo yake mahakamani.

Lissu amepanga kuleta mashahidi 12 kwa ajili ya utetezi dhidi yake akiwemo na yeye mwenyewe huku, wengine wakiwa ni Viongozi wakuu wa serikali na Chama chake.

Hii leo baada ya Lissu kuhitimisha kujitetea anatarajia kumuita shahidi mwingine kutoka kwenye chama chake akiwa kama shahidi namba mbili wa utetezi.

Kesi inaendelea