Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amemaliza kutoa ushahidi wake katika kesi ya uhaini inayomkabili, akisisitiza mbele ya Mahakama Kuu kwamba upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kwamba alitenda kosa hilo.

Katika sehemu ya mwisho ya utetezi wake, Lissu amejikita katika kuhoji aina ya mashahidi waliotolewa na upande wa mashtaka, uzito wa ushahidi wao, namna upelelezi ulivyofanyika pamoja na mazingira ya kukamatwa kwake.
Lissu amesema anataka kujikita katika ushahidi huo kama ilivyowasilishwa na upande wa mashtaka, akieleza kuwa ushahidi wake unalenga kuonyesha kwamba hakuna kosa la uhaini wala kosa jingine la jinai alilotenda.
Lissu ameiambia Mahakama kwamba wakati wa hatua ya awali ya kesi, upande wa Jamhuri uliwasilisha orodha ya mashahidi 30 ambao ulisema wangetumika kuthibitisha tuhuma za uhaini.
Hata hivyo, amesema ni mashahidi 17 pekee walioletwa mahakamani, huku wengine 13 wakiwa hawakuitwa kutoa ushahidi.
Kwa mujibu wa Lissu, kati ya mashahidi hao 17, wanane ni maofisa wa Jeshi la Polisi na tisa ni mashahidi waliolindwa ambao utambulisho wao haukuwekwa wazi hadharani.
Amesema hali hiyo inamaanisha kuwa Mahakama na upande wa utetezi hawakufahamu majina yao halisi, wanapoishi wala wanachofanya, zaidi ya majina ya utambulisho waliyopewa kama P1 na wengine.
Lissu amesema ushahidi wa mashahidi hao unapaswa kutazamwa kwa umakini kutokana na mazingira ambayo uliwasilishwa.
Akizungumzia ushahidi wa shahidi wa kwanza, George Bagemu, Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Kanda, Lissu amesema shahidi huyo aliongoza timu ya upelelezi kati ya Aprili 4 na 8, mwaka 2025, siku moja kabla ya kukamatwa kwake.
Amesema katika mahojiano yake, Bagemu alikiri kwamba wakati huo alikuwa akiwasiliana moja kwa moja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI Ramadhani Kingai.
Lissu amesema alimuuliza Bagemu kama aliwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Kanda, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Ofisi ya Usalama wa Taifa au Afisa Usalama wa Mkoa, lakini shahidi huyo alisema hakufanya hivyo.
Kwa mujibu wa Lissu, mtu aliyethibitishwa kuwa kiungo katika upelelezi huo alikuwa Kingai, kupitia aliyekuwa Naibu Kamishna wa Polisi, Ramadhani Ng’anzi.
Lissu pia amerejea ushahidi wa shahidi huyo kuhusu kukamatwa kwake, akisema Bagemu alieleza kuwa hakutoa amri ya kukamatwa kwake na hakujua ni nani aliyetoa amri hiyo.
Amesema Bagemu alieleza kwamba alipokea taarifa kutoka kwa DCP Ng’anzi kwamba mtuhumiwa alikuwa amekamatwa Mbinga na alikuwa akisafirishwa kwenda Dar es Salaam.
-Ahoji uhusiano wa polisi na kesi yake-
Lissu amedai kuwa ushahidi wa Bagemu pamoja na wa shahidi wa 16, ACP Amini Mahamba, unaonyesha namna maofisa wa polisi walivyohusika katika upelelezi wa kesi hiyo.
Amesema ushahidi wa maofisa hao unapaswa kuangaliwa kwa umakini kwa sababu, kwa mtazamo wake, baadhi yao wamekuwa wakihusika katika kesi na hatua mbalimbali za kisheria dhidi yake kwa miaka mingi.
Lissu amemtaja DCI Ramadhani Kingai na IGP Camilius Wambura, akidai kuwa wamekuwa sehemu ya kile alichokiita mkakati wa muda mrefu wa kumfungulia mashtaka na kumweka gerezani.
Akigeukia mashahidi ambao si maofisa wa polisi, Lissu amesema saba kati yao walitoa maelezo ya maandishi kwa polisi na pia wakatoa ushahidi mbele ya Mahakama.
Kwa mujibu wa Lissu, mashahidi hao walieleza kwamba walikuwa wamepanga kufanya vitendo vya uhalifu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Amesema ushahidi huo wa maandishi, kwa mtazamo wake, unamsaidia badala ya kumtia hatiani.
Lissu amesema mashahidi hao walikamatwa kati ya Aprili 4 na 8, 2025, wakidaiwa kupanga vitendo hivyo, na baadaye walikubali kuwa mashahidi dhidi yake baada ya kuahidiwa kuondolewa mashtaka yaliyokuwa yanawakabili.
Amesema mmoja wa mashahidi hao alieleza kuwa alikubali kuwa shahidi baada ya kupewa ahadi kwamba mashtaka dhidi yake yangeondolewa.
Lissu amehoji uzito wa ushahidi wa watu ambao, kwa maelezo yake, walikiri kupanga uhalifu na kisha wakafutiwa mashtaka baada ya kuwa mashahidi wa Jamhuri.
-Ahoji mauaji ya baada ya uchaguzi-
Katika hoja nyingine, Lissu amezungumzia maeneo ambayo baadhi ya mashahidi hao walitoka, akirejea pia takwimu za mauaji zilizotolewa na Tume ya Uchunguzi iliyoongozwa na Jaji Mohamed Chande.
Amesema baadhi yao walitoka Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Songea, maeneo ambayo, kwa mujibu wa taarifa ya Tume hiyo, yaliripotiwa kuwa na vifo wakati wa vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi.
Lissu amesema ACP Amini Mahamba, ambaye alikuwa miongoni mwa maofisa waliohusika katika upelelezi, aliulizwa kama polisi waliwafuatilia au kuwachukulia hatua waliohusika na mauaji hayo, lakini jibu lilikuwa hapana.
Kutokana na hilo, amehoji uzito wa ushahidi wa watu hao katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Lissu amesema shtaka linalomkabili linahusisha madai kwamba alikuwa na nia ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kwamba alidhihirisha nia hiyo kupitia kauli alizotoa.
Amesema katika kesi ya uhaini, jambo la kwanza ambalo upande wa mashtaka unapaswa kuthibitisha ni uwepo wa nia ya kutenda kosa hilo.
Amesema mashahidi waliotumika kujaribu kuthibitisha suala hilo ni pamoja na Inspekta Kaaya, George Bagemu na ACP Amini Mahamba.
Kwa mujibu wa Lissu, Bagemu alidai kuwa aliona nia hiyo kupitia kauli ambazo alidai Lissu alitoa kuhusu kuzuia uchaguzi.
Hata hivyo, Lissu amesema shahidi wa 17, ambaye alisema alikuwepo kwenye mkutano uliotajwa katika kesi hiyo, hakushuhudia kauli yoyote ya kijinai au ya kihaini.
Lissu amesema ushahidi kuhusu kauli zinazodaiwa kuwa za kihaini una mkanganyiko mkubwa.
Amesema mashahidi kadhaa wa upande wa mashtaka walidai kwamba yeye ndiye aliyechapisha video yenye kauli hizo, lakini shahidi wa 17, ambaye kwa mujibu wa Lissu ndiye aliyekuwepo katika mkutano huo, alisema hakusikia kauli ya kijinai wala ya kihaini.
Lissu amesema shahidi huyo pia alieleza kuwa yeye ndiye aliyepiga picha katika mkutano huo pamoja na wenzake na kwamba walihifadhi video hiyo kwenye mtandao wa Jambo TV.
Lissu pia ameiambia Mahakama kwamba wakati wa hatua ya awali ya kesi, upande wa Jamhuri uliahidi kuwasilisha vielelezo 11, vikiwemo vielelezo tisa vya maandishi na viwili visivyo vya maandishi.
Hata hivyo, amesema hakuna hata kimoja kati ya vielelezo hivyo kilichowasilishwa, akisisitiza kwamba Jamhuri imebaki na maelezo ya mashahidi pekee.
-Asema upelelezi haukuhusisha DPP-
Katika hoja nyingine, Lissu amehoji namna upelelezi wa kesi hiyo ulivyofanyika, akisema sheria inampa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mamlaka ya kusimamia na kuelekeza upelelezi wa makosa ya jinai.
Amesema alipowauliza mashahidi wa polisi nani alisimamia upelelezi wa kesi hiyo, hawakuweza kutoa jibu la moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Lissu, shahidi wa kwanza na wa 16 walithibitisha kwamba hakukuwa na mwakilishi wa DPP aliyeshiriki katika upelelezi huo kwa namna aliyodai inavyotakiwa kisheria.
Amesema hali hiyo inaonyesha kuwa upelelezi wa kesi hiyo haukufanyika kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa.
Lissu pia amerejea siku aliyokamatwa katika mji wa Mbinga, mkoani Ruvuma, Aprili 9, 2025.
Amesema alikamatwa baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara na kwamba kabla hajashuka jukwaani alifuatwa na aliyemtaja kuwa OCD wa Mbinga.
Kwa mujibu wa Lissu, afisa huyo alimwambia aende kituoni lakini hakumweleza kosa alilokuwa amefanya.
Lissu amesema alikataa kuondoka hadi aelezwe sababu ya kukamatwa kwake, lakini baadaye mabomu ya polisi yalianza kulipuliwa na vurugu zikazuka.
Amesema alijikuta akiwa ndani ya gari la polisi na baadaye akapelekwa kituo cha polisi Mbinga.
Akiwa huko, amesema alikutana na aliyemtaja kuwa OC-CID, Rugamo Gwasa, ambaye alimweleza kwamba walikuwa wamepewa amri ya kumkamata kutoka kwa RPC lakini hawakuambiwa kosa alilokuwa amefanya.
Lissu amesema baadaye alipelekwa Songea na kukutana na RPC Chilya, ambaye, kwa mujibu wake, alimweleza kuwa walikuwa wakitekeleza maelekezo kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma ya kumpeleka Dar es Salaam.
Lissu amesema baadhi ya maofisa aliowataja kama waliohusika katika mchakato wa kukamatwa kwake walikuwa kwenye orodha ya mashahidi wa Jamhuri lakini hawakuitwa kutoa ushahidi.
Ametaja ACP Rugamo Gwasa na ASP Charles Makunja, akisema kama wangeitwa, angeweza kuwahoji kuhusu mazingira ya kukamatwa kwake na kama taratibu za kisheria zilifuatwa.
-Ahoji tofauti kati ya maelezo ya polisi na ushahidi wa mahakamani-
Lissu amemalizia kwa kuhoji tofauti kati ya maelezo ya mashahidi waliyoandika polisi na ushahidi walioutoa mbele ya Mahakama.
Amesema mashahidi wote 17 wa upande wa mashtaka waliwahi kutoa maelezo polisi, huku 16 kati yao wakiwa na maelezo ambayo, kwa mujibu wa Lissu, yamekuwa sehemu ya ushahidi wa utetezi.
Amesema mashahidi hao walipotoa ushahidi wa mdomo mahakamani waliongeza mambo ambayo hayakuwepo katika maelezo yao ya awali.
Kwa mtazamo wake, ushahidi wa mdomo unaokinzana na ushahidi wa maandishi katika jambo lilelile haupaswi kuaminiwa.
Amesema hali hiyo inaifanya Mahakama kuwa na sababu ya kuhoji uaminifu wa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.
Katika hitimisho lake, Lissu amesisitiza kwamba baadhi ya maofisa wa polisi waliandika wenyewe maelezo yao ya polisi na baadaye wakaja kuyathibitisha wenyewe mahakamani.
Amesema alipowauliza ni sheria gani inayowaruhusu kufanya hivyo, baadhi yao walijibu kuwa hiyo ndiyo namna polisi wanavyofanya kazi.
Lissu amesema ni shahidi mmoja tu kati yao ambaye, kwa mujibu wake, alitoa maelezo yake mbele ya polisi mwingine kama inavyotakiwa.
Amesema kutokana na mapungufu hayo, anadai ushahidi wa upande wa mashtaka hauaminiki.
Lissu amehitimisha utetezi wake kwa kuwaambia majaji kwamba ushahidi alioutoa unaonyesha kuwa upande wa Jamhuri haujathibitisha vipengele muhimu vya kosa la uhaini, ikiwemo kuwepo kwa nia ya kutenda kosa hilo.
“Nimemaliza,” amesema Lissu baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake mbele ya Mahakama.
Kesi imeahirishwa kwa muda