Mashahidi watatu wa utetezi ambao Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, iliamuru waitwe kutoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu,imeelezwa kuwa wako nje ya nchi, hali iliyosababisha kesi hiyo kuahirishwa hadi Ijumaa, Septemba 18, 2026.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano, Septemba 16, 2026, baada ya shahidi wa tano wa upande wa utetezi, John Heche, kumaliza kutoa ushahidi wake uliodumu kwa siku sita.
Lissu, ambaye anajitetea mwenyewe katika kesi hiyo, aliliambia Mahakama kuwa baada ya maelekezo yaliyotolewa awali, aliwasiliana na Msajili wa Mahakama ili kufuatilia utekelezaji wa wito kwa mashahidi watatu ambao Mahakama iliamuru waitwe.
Kwa mujibu wa taarifa aliyopewa na Msajili, mashahidi hao wote watatu walipatiwa wito katika mchakato uliofanyika Dodoma, lakini haikuwezekana kuwapatia nakala za wito kwa sababu walikuwa nje ya nchi.
Mashahidi hao ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali John Mkunda, na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura.
Lissu alieleza kuwa kwa mujibu wa taarifa aliyopokea kutoka kwa Msajili, Kingai anatarajiwa kurejea nchini leo Jumatano, Septemba 16, 2026.
Alisema pia Msajili amemueleza kuwa Kamishna wa Polisi anatarajiwa kuwepo mahakamani siku ya Ijumaa kwa ajili ya kutekeleza wito uliotolewa na Mahakama kwa Kingai.
Hata hivyo, kuhusu mashahidi wengine wawili, Jenerali Mkunda na IGP Wambura, Lissu alisema bado haijulikani watarudi lini nchini.
Kutokana na hali hiyo, Lissu aliiomba Mahakama kuahirisha kesi hadi Ijumaa saa 8:00 mchana, akieleza kuwa muda wa asubuhi utampa nafasi ya kumuandaa shahidi anayetarajiwa kufika, pamoja na kuchukua maelezo yake huku akisisitiza kuwa hawezi kumuhoji shahidi kama hajamuandaa kwa hofu ya shahidi kumgeuka au akawa shahidi adui.
Lissu alisema kwa upande wa mashahidi ambao bado hawajulikani watarudi lini, wataendelea na shahidi aliyepo na baadaye watafanya uamuzi kuhusu hatua ya kuchukua iwapo mashahidi hao hawatafika.
Aidha, Lissu aliiambia Mahakama kuwa anatambua ratiba ya kesi hiyo na anatamani mchakato wa ushahidi ukamilike ili pande zote zifikie hatua ya kutoa hoja za mwisho kabla ya majaji kuanza kufanya uamuzi wa kesi.
“Kwa hiyo kama watakuwa wanakuja basi hatutachukua muda mrefu. Na wasipokuja kabisa, maana yake itakuwa ni juu ya Mahakama,” alisema Lissu.
Kwa upande wake, Wakili wa Jamhuri, Nassoro Katuga, alisema upande wa mashtaka hauna pingamizi dhidi ya ombi la kuahirishwa kwa kesi hiyo, lakini uliitaka Mahakama kumtaka Lissu kuhakikisha mashahidi wake wanapatikana kwa wakati.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa, Septemba 18, 2026, saa 8:00 mchana.
Lissu anashtakiwa kwa kosa la Uhaini ambaye anadaiwa kuitishia Serikali kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu.
Alikamatwa Aprili 9, 2025, wilaya tab Mbinga, Mkoa wa Ruvuma, wakati wa kampeni ya Chadema ya “No Reforms, No Election” na amekana mashtaka yanayomkabili.