Lissu: Kingai Amesema Hawezi Kunitetea

Mshatakiwa katika kesi ya uhaini, Tundu Lissu, ameieleza Mahakama kwamba shahidi wake wa utetezi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai, amegoma kutoa ushahidi kwa upande wake licha ya kufika mahakamani baada ya kupokea wito.

Lissu: Kingai Amesema Hawezi Kunitetea

Lissu amesema hayo leo Septemba 18, 2026, wakati akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzania, akisema alikutana na DCI Kingai mapema leo katika chumba cha mahakama ili kumweleza maeneo ambayo alitarajia shahidi huyo ayazungumzie katika ushahidi wake.Kwa mujibu wa Lissu, baada ya mazungumzo hayo, Kingai alimweleza kuwa hayuko tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi, akisema yuko upande wa watu wanaotamani Lissu apatikane na hatia na atafurahi kusikia hilo.“Waheshimiwa majaji, kwanza naomba kutoa taarifa kwamba nimekutana na Kamishna Ramadhani Kingai, ambaye nimekuwa nimependekeza awe shahidi wangu wa leo. Nimekutana naye mahakamani kwenye chumba hiki hiki.“Waheshimiwa majaji, kwa hiyo naweza kuthibitisha kwamba ameheshimu wito wa Mahakama, amekuja na nimezungumza naye kuhusu suala la yeye kuwa shahidi wa upande wa utetezi. Nimezungumza naye kwa kiasi kirefu na baada ya kuzungumza naye na kumweleza maeneo ambayo ningependa atoe ushahidi, Kamishna Kingai akasema yeye hawezi na hayuko tayari kutoa ushahidi kwa upande wangu.“Kwa maneno yake mwenyewe amesema yeye yuko upande wa wale wanaomba na watakaoshangilia nikipatikana na hatia. Kwa hiyo amesema hayuko tayari kuja kutoa ushahidi kwa niaba yangu,” amesema Lissu.Lissu amesema kutokana na msimamo huo wa Kingai, ameamua kutomlazimisha kutoa ushahidi ambao hataki kuutoa.Ameendelea kueleza kuwa Kingai pia ametoa msimamo kuhusu mashahidi wengine wawili ambao Mahakama iliamuru wapelekwewe wito, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda, na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camilius Wambura.Kwa mujibu wa Lissu, Kingai amesema hata CDF. Nkunda na IGP.Wambura watakapopokea wito wa Mahakama, msimamo wao utakuwa sawa na wake, kwamba hawatakuwa tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi kwa sababu wako upande wa wanaotamani na kushangilia Lissu apatikane na hatia.“Waheshimiwa majaji, Kamishna wa Polisi Kingai amesema kitu kingine kuhusiana na mashahidi wengine wawili ambao Mahakama hii iliamuru wapelekwe wito, yaani General Jacob Nkunda na IGP Camilius Wambura.“Kuuhusiana na hao, Waheshimiwa majaji, Kamishna wa Polisi Kingai amesema vile vile hata wao watakapopata wito wa Mahakama, msimamo wao utakuwa huo huo kwamba na wao hawatakuwa tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi kwa sababu ile ile kwamba wako upande wa wale wanaombea na kushangilia nikipatikana na hatia,” amesema.Lissu amesema kutokana na hali hiyo, hana mashahidi wengine wa kuwaita na hivyo kuomba Mahakama ifunge rasmi ushahidi wa upande wa utetezi.“Katika mazingira haya, Waheshimiwa majaji, maana yake ni kwamba sina mashahidi zaidi na kwa hiyo naomba kufunga ushahidi wa upande wa utetezi.“Ni hayo tu, Waheshimiwa majaji.”Baada ya kufunga ushahidi wa upande wa utetezi, Lissu pia ameomba Mahakama ipange tarehe ya kuwasilishwa kwa hoja za mwisho za pande zote mbili, akieleza kuwa kwa hatua hiyo kesi imefikia mwisho wa ushahidi kwa pande zote.“Waheshimiwa majaji, kwa vile sasa kesi kwa pande zote mbili imefungwa, naomba Mahakama itupangie siku ya kuja kuwasilisha hoja za pande zote mbili, Waheshimiwa majaji.“Waheshimiwa majaji, naelewa kwamba ratiba ya Session hii inaisha tarehe 25, Ijumaa ijayo, kwa hiyo tuna siku saba.“Sasa, Waheshimiwa majaji, kesi hii hapa nina karibu kurasa 1,000 za submissions. Pendekezo langu itabidi tufanye kazi kubwa sana upande wangu na mashtaka na upande wangu. Mimi naweza nikasema nitakuwa tayari kufanya final submissions siku ya Jumatano.”Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini katika Mahakama Kuu ya Tanzania, akidaiwa kutenda kosa la kuitishia Serikali kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16, Rekebisho la mwaka 2023.Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, akiwa raia wa Tanzania na kwa nia ya uchochezi, alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kutamka na kuchapisha mtandaoni maneno yaliyodaiwa kuwa ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania.Maneno hayo yanayodaiwa kuwa ya uhaini ni pamoja na: “Wanasema kitu kimoja hapa, msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”Baada ya hoja za pande zote kukubaliana Mahakama imeahirisha shauri hilo hadi Jumatano Septemba 23,2026 saa tatu asubuhi.