Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini Tanzania (CHADEMA) Tundu Lissu, ametangaza rasmi nia ya kugombea nafasi ya uenyekiti taifa wa chama hicho.
Akizungumza jijini Dar es Salaam siku ya Disemba 12, mwanasiasa huyo amesema kuwa alimuandikia Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, kuonesha nia yake ya kutokugombea tena nafasi ya Umakamu Mwenyekiti, kama alivyotangaza mwezi Agosti 2024.
”Ninapenda kuamini kwamba, ninyi wanachama wenzangu mnaamini nina sifa za kutosha za kugombea nafasi ya juu ya uongozi katika chama chetu” amesema Lissu
Lissu ameongeza kusema ”Nimemuandikia barua rasmi katibu mkuu kujiondoa katika kinyang’anyiro cha kuwania umakamu mwenyekiti, baada ya kutangaza nia hiyo tarehe 6, Agosti 2024,”
“Badala yake, nimewasilisha nia yangu ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa taifa katika uchaguzi wa mkuu wa chama,” aliongeza.
Hatua hiyo inakuja huku kukiwa na vuguvugu kubwa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania ya kupata uongozi mpya na uelekeo wa kimkakati wa kuondoa utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini humo.
Kwa sasa, nafasi ya uenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania inashikiliwa na Freeman Mbowe, huku Tundu Lissu akiwa Makamu wake. Mbowe amekuwa mwenyekiti wa Chadema kwa zaidi ya Miaka 20