Patrice Emery Lumumba, ambaye mabaki yake yalirejeshwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wiki iliyopita, alijipatia umaarufu Juni 30, 1960 katika hotuba yake kali dhidi ya ukoloni wa zamani wa Ubelgiji.
Mbele ya Mfalme Baudouin wa Ubelgiji, waziri mkuu huyo mwenye umri wa miaka 34 aliwashutumu watawala hao wa zamani wa kikoloni kwa unyanyasaji wa kibaguzi na kulazimisha “utumwa wa kudhalilisha” kwa watu wa Kongo, hotuba hiyo ilimfanya Lumumba kuwa shujaa wa papo hapo wa harakati za uhuru wa Afrika.
“Tulikumbana na kashfa, matusi, vipigo ambavyo tulipitia asubuhi, mchana na jioni, kwa sababu tulikuwa watu weusi,” alitangaza.
Lilikuwa ni jibu madhubuti kwa Mfalme Baudouin ambaye hotuba yake muda mfupi kabla ilikuwa imesalimu kazi ya babu yake mfalme Leopold II, akisisitiza kwamba yeye hakuwa ‘mkoloni’ bali amekuja kwa ‘misheni yakuwastaarabisha waafrika.’
Lumumba alizaliwa Julai 2, 1925 katika kijiji cha Onalua katika jimbo la kati la Sankuru, wazazi wake walikuwa kutoka kabila la Tetela.
Alianza masomo yake kwa kusomea uuguzi, kisha akajiunga na shule ya posta ya utawala wa kikoloni, na kuhitimu kuwa karani katika huduma ya barua katika jiji la kaskazini-mashariki la Stanleyville, ambalo sasa linaitwa Kisangani.
Alishtakiwa kwa ubadhirifu na akahukumiwa kifungo cha miezi kadhaa jela mwaka wa 1956. “Nilifanya nini zaidi ya kurudisha kidogo pesa ambazo Wabelgiji waliiba kutoka Kongo?” anaripotiwa kusema wakati huo.
“Hakuwahi kukataa kutumia fedha kwa kazi zingine” alisema msomi kutoka Kongo, Emmanuel Kabongo, ambaye ameandika sana kuhusu Lumumba.
Baada ya kutoka gerezani “kutokana na uhusiano wake na Wabelgiji waliberali,” aliajiriwa kama mkurugenzi wa kibiashara wa kiwanda cha bia kilichotaka kuongeza mauzo yake ya bia huko Leopoldville, jiji ambalo sasa linaitwa Kinshasa, alisema.
Akiwa posta alikuwa alikuwa akilipwa francs 3,000 pekee za Ubelgiji, ghafla alikuwa akilipwa franc 25,000 kwa kazi yake mpya, Kabongo alisema.
Mwaka 1958 alizindua chama cha kisiasa, Congolese National Movement (MNC), kilichotaka uhuru na taifa la Kongo.
Wakosoaji wake walimshutumu kuwa mkomunisti, lakini msomi wa Kongo Jean Omasombo alisema hakuwa.
“Alisema mara kadhaa alikuwa mzalendo, sio mkomunisti,” alisema.
Kwa mwezi mmoja mwanzoni mwa 1960, Lumumba alishiriki katika mazungumzo kuhusu uhuru wa Kongo mjini Brussels, pamoja na wanasiasa wengine wa Kongo na viongozi wa kitamaduni.
Chama chake kilishinda uchaguzi wa kitaifa mnamo Mei 1960, mwezi mmoja kabla ya uhuru, na akatajwa kama waziri mkuu wa kwanza wa nchi hiyo ilipopata uhuru.
Alikuwa miongoni mwa viongozi wa Afrika walioongoza kukomesha ukoloni barani Afrika mwishoni mwa miaka ya 1950.
Lakini, anasema Kabongo, “alikuwa tu mkuu wa serikali ya jimbo jipya kwa miezi miwili na siku kumi na tatu,” kuanzia Juni 30 hadi Septemba 12, 1960.
Hotuba ya uhuru ya mwanasiasa huyo shupavu ilichukiza sana Ubelgiji.
Mataifa ya Magharibi hayakuhitaji kitu kingine chochote kumwona kijana huyo mwenye umri wa miaka 35 kama tishio, hasa baada ya kutafuta kuungwa mkono na Umoja wa Kisovieti.
Kwa lengo la kumzuia, Ubelgiji na CIA walitumia tamaa ya viongozi wengine wa Kongo, nyaraka zinaonyesha.
Walifanikiwa kumtumia mkuu wa jeshi aliyeitwa Joseph-Desire Mobutu, aliyeongoza mapinduzi yaliyomng’oa Lumumba.
Baadaye Mobutu angenyakua madaraka katika mapinduzi mengine na kuweka utawala wa kidikteta kuanzia 1965-1997, na kubadilisha jina la nchi hadi Zaire na yeye mwenyewe akajiita Mobutu Sese Seko.
Baada ya Lumumba kuondolewa madarakani, alikamatwa na kukabidhiwa kwa mamlaka na kunyongwa katika jimbo lenye utajiri wa madini kusini-mashariki mwa Katanga. Jimbo ambalo lilijitenga na taifa hilo changa miezi kadhaa baada ya uhuru kwa msaada wa Ubelgiji.
Ndege ilitua katika uwanja wa ndege wa mji mkuu wa jimbo la Katanga Elisabethville — sasa unaitwa Lubumbashi — mwanzoni mwa 1961.
Alifukuzwa hadi msituni na kupigwa risasi na kufa chini ya mti na watu waliotaka kujitenga wa Katanga na mamluki wa Ubelgiji pamoja na wenzake wawili baada ya kuingia usiku wa Januari 17, 1961. Alikuwa na umri wa miaka 35 tu.
Mwili wake uliyeyushwa kwa tindikali, lakini afisa wa polisi wa Ubelgiji aliyehusika katika mauaji hayo aliweka jino lake moja kama zawadi.
Ubelgiji hatimaye aliirudisha kwa familia yake Jumatatu wiki iliyopita.
Hotuba ya Lumumba katika siku ya uhuru wa taifa, ilifunga hatima yake,” alisema Kabongo.
“Lakini utaifa wake na ukaribu wake na watu wengine waliokuwa wakipigania uhuru wa nchi zao … ulikuwa umevuruga tamaa ya Marekani nchini Kongo,” aliongeza.