Serikali ya taifa la Togo imethibitisha kuwa kiongozi wa Bukina Faso aliyeenguliwa lutein kanali Paul Henri Sandaogo Damiba amekimbilia nchini humo baada ya mapinduzi ya kijeshi.
Waziri wa mawasiliano ambaye ndiye msemaji wa serikali nchini Togo Akodah Ayewouadan amesema Damiba yuko Togo kama njia kuonyeshesha kujitolea kwa taifa hilo kuhakikisha kuna amani katika eneo hilo.
Mitaa ya mji mkuu wa Burkina Faso Ouagadougou imesalia kimya jumatatu baada ya siku mbili ya makabiliano kati ya makundi mbili hasimu ya kijeshi.
Walisema kiongozi mpya wa nchi hiyo aliyejitangaza, Kapteni Ibrahim Traoré, alilazimisha kujiuzulu kwa Luteni Kanali Paul-Henri Damiba na masharti aliyoweka.
Tangazo hilo lilifuatia mashambulizi dhidi ya taasisi za Ufaransa, baada ya kuripotiwa kuwa Lt Kanali Damiba alikuwa akihifadhiwa katika kambi ya kijeshi ya Ufaransa.
Ni mapinduzi ya pili mwaka huu. Katika visa vyote viwili, hali mbaya ya usalama nchini humo na kushindwa kukabiliana na waasi wa Kiislamu kulilaumiwa kwa unyakuzi huo.
Inadaiwa kuwa Burkina Faso inadhibiti kidogo kama 60% ya eneo lake na ghasia za makundi ya kigaidi zinazidi kuwa mbaya.
Umoja wa Afrika umetaka kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba ifikapo Julai 2023, ukikubaliana na jumuiya ya kikanda ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas) kwamba kuondolewa madarakani kwa kiongozi Lt Kanali Damiba kulifanywa kinyume na katiba.
Jumuiya ya Ecowas awali ilisema kwamba haikuwa sawa kwa waasi wa jeshi kunyakua mamlaka wakati nchi hiyo inaelekea kutwaa uongozi kwa raia.
Hakujatolewa taarifa kamaili na kiongozi huyo aliyepinduliwa ila viongozi wa kidini na jumuiya walisema kuwa kiongozi huyo wa kijeshi ambaye alitimuliwa katika mapinduzi siku ya Ijumaa, alikubali kuachia ngazi kabla ya kuelekea nchini Togo.
Walisema Luteni Kanali Damiba aliweka masharti saba ya kuachia ngazi – ikiwa ni pamoja na hakikisho la usalama wake, makubaliano ya kuendelea na juhudi za maridhiano ya kitaifa na kuendelea kuheshimu dhamana ya kurejea kwa utawala wa kiraia ndani ya miaka miwili.
Kanali aliyeng’olewa madarakani alimwondoa mwenyewe madarakani Rais Roch Kaboré mnamo Januari, akisema kwamba ameshindwa kukabiliana na ongezeko la ghasia za wanamgambo wa Kiislamu.
Raia wengi nchini Burkina Faso hawajahisi kuwa salama kwa muda. Uasi wa Kiislamu ulizuka nchini humo mwaka wa 2015, na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na kuwalazimisha takriban watu milioni mbili kutoka makwao.
Burkina Faso imekumbwa na mapinduzi manane tangu uhuru mwaka 1960.