Ukaguzi wa sajili ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) uligundua maafisa wasimamizi wa uchaguzi (returning officers) kumi na nne (14) na zaidi ya wapiga kura milioni 2 wasiotambulika. Maafisa hao walikuwa wakiendesha Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Takwimu wa IEBC (IDMS).
Kulingana na ripoti ya kampuni iliyofanya ukaguzi huu, KPMG, stakabadhi bandia zilitumika kujiandikisha huku zingine zikisajiliwa mara mbili katika chaguzi zilizopita.
Ripoti hiyo ilifichua kuwa maafisa hewa walikuwa na idhini ya kuhamisha, kufuta, kuingiza, kubadilisha na kuhuisha daftari la wapiga kura.
Katika ripoti ya kina, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati alisema, tume hiyo imechapisha vituo vyote vya kupigia kura kwenye uchapishaji rasmi wa serikali ya Jamhuri ya Kenya, na hitlafu zote zilizobainishwa na ukaguzi huu zilishughulikiwa.