Hifadhi ya wanyama ya Serengeti nchini Tanzania imeshinda tuzo ya kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa mwaka 2021.Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa hifadhi hiyo ya Serengeti kushinda tuzo hiyo baada ya kushinda tena mwaka wa 2019 na 2020.
Mbuga ya wanyama ya Maasai Mara ilioko Kenya na inapakana na mbuga ya Serengeti Tanzania ilishinda tuzo hiyo ya kuwa hifadhi bora barani Afrika mfululizo kutoka mwaka wa 2014 hadi 2018.
Tuzo hizo hutolewa na taasisi ya World Travel Awards (WTA) ya nchini Marekani.
Mbuga hizi mbili kila mwaka hushuhudia maajabu makubwa ya dunia. Kulingana na watafiti kuvuka kwa nyumbu katika mto Mara kutoka hifadhi ya Serengeti hadi ya Maasai Mara imeorodheshwa nambari nane katika orodha ya Maajabu Makubwa ya Dunia.
Uhamiaji mkubwa wa nyumbu kutoka mbuga moja hadi nyingine ndio uhamiaji mkubwa zaidi wa wanyama duniani. Zaidi ya nyumbu milioni moja, punda milia 300,000 na paa huhama kutoka mbuga ya Serengeti hadi Maasai Mara katika mzunguko wa kila mwaka, wanyama hao wakitafuta malisho na maji.
Uhamiaji wa wanyama huanzia katika hifadhi ya Ngorongoro kusini mwa Serengeti nchini Tanzania na kuzunguka hadi mbuga ya Serengeti na kueleka kaskazini katika mbuga ya wanyama ya Masaai Mara nchini Kenya.
Awamu ya kwanza huanzia mwezi wa Januari hadi Machi, wakati msimu wa kuzaa unapoanza na kuna nyasi na maji ya kutosha kwa zaidi ya nyumbu 1.7 milioni na punda milia 300,000 na paa 470,000.
Mvua inapoisha mwezi Mei, wanyama hao huanza kuelekea kaskazini magharibi, ifikiapo mwezi wa Julai wanyama hao hukusanyika katika mto Grumeti/Mara tayari kuvuka na kueleka katika mbuga ya wanyama ya Maasai Mara.
Wanyama hao hukaa katika mbuga ya Masaai Mara hadi mwisho wa mwezi Oktoba, mapema mwezi Novemba wakati mvua inapoanza wanyama hao huelekea kusini tena katika hifadhi ya Serengeti na kuzaa watoto wao mapema mwezi Februari.
Takriban nyumbu 250,000 hufariki katika safari yao wanapovuka mto Mara kutokana na kuliwa na simba na mamba, nyumbu wengine hufariki kutokana na njaa na kiu na hata uchovu kwa jumla inakuwa safari ndefu kwa wanyama hao, takriban 1000 KM, kutoka mbuga moja hadi nyingine mwaka mzima.
Kuvuka kwa wanyama hao kutoka Serengeti hadi Mara mwezi Oktoba huwa kivutio kikubwa kwa watalii.