Polisi wa Nigeria siku ya Jumatatu waliutawanya umati wa watu wenye hasira uliokuwa ukimtafuta mwanamke waliyemtuhumu kwa kutoa matamshi ya kukufuru dhidi ya Mtume Muhammad, katika mji wa Maiduguri ulio na Waislamu wengi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Maandamano hayo, ambayo wakaazi na chanzo cha usalama walisema hayakuwa na vurugu, yalifanyika siku chache baada ya mwanamke mwingine kushutumiwa kwa kukufuru na kuuawa na kundi la watu kaskazini magharibi mwa jimbo la Sokoto.
Wakaazi watatu waliiambia AFP kwa njia ya simu kwamba karibu watu 300 walivamia kitongoji anachoishi mwanamke huyo katika viunga vya mji mkuu wa jimbo la Borno siku ya Jumatatu.
Umati ulikuwa unamtafuta, lakini hawakuweza kumpata, walisema.
“Polisi waliwafukuza waandamanaji,”mkaazi Abdulkarim Adam aliambia AFP.
“Polisi hawakumkamata mtu, waliwatawanya tu kwa kuwafyatulia risasi hewani na kurusha mabomu ya machozi,” alisema Adam katika taarifa iliyoungwa mkono na wakazi wengine wawili, Bunu Mustapha na Musa Grema.
Chanzo cha usalama kilichoomba kutotajwa jina kiliiambia AFP tukio hilo lilihusisha umati mkubwa ambao walikuwa wakaidi lakini hawakuwa na vurugu.
Mkuu wa polisi wa eneo hilo Abdu Umar hakuthibitisha maelezo ya maandamano hayo lakini aliwaambia waandishi wa habari kwamba walikuwa wamepokea ripoti kwamba ‘baadhi ya waru wanapanga kuvuruga amani iliyopo’ katika jimbo hilo.
Alisema inahusishwa vurugu ilioanzishwa na mauaji ya Alhamisi iliyopita ya mwanamke anayeshutumiwa kwa kukufuru huko Sokoto.
Alipigwa mawe hadi kufa na mwili wake kuchomwa moto na umati wa watu baada ya kuona kwamba maoni aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii yalimkashifu Mtume.
Maandamano yalizuka Sokoto siku ya Jumamosi kufuatia kukamatwa kwa washukiwa wawili, polisi wa Sokoto walisema, na serikali ikaweka amri ya kutotoka nje kwa muda.
Kukashifu ni suala nyeti nchini Nigeria, taifa lenye watu wengi zaidi barani Afrika ambalo watu milioni 210 wamegawanyika takriban sawa kati ya Waislamu na Wakristo.