Maelfu ya watu waliingia mitaani nchini Burundi Jumamosi wakiunga mkono serikali baada ya Umoja wa Ulaya na Amerika kurejesha misaada kwa taifa hilo la Afrika ya kati.
Brussels na Washington zote zilitaja maendeleo ya kisiasa chini ya Rais Evariste Ndayishimiye ikiwa sababu yao ya kufanya maamuzi ya kuondoa vikwazo dhidi ya Burundi — ingawa makundi ya haki za kibinadmu yanasisitiza haki za binadamu bado zinadhulumiwa pakubwa.
Hamza Venant Burikukiye, mjumbe wa mashirika ya kiraia aliye karibu na serikali, akizungumza kwa niaba ya walioandaa maandamano, alisema waandamanaji hao walitaka kuishukuru EU na Amerika kwa kuondolewa kwa vikwazo “visivyo vya haki.”
Waandalizi walisema maelfu ya watu walijitokeza katika mji mkuu Bujumbura, huku maandamano mengine pia yakifanyika katika maeneo mengine ya nchi.
Burundi ilitumbukia katika machafuko mabaya mwaka 2015 wakati rais wa wakati huo Pierre Nkurunziza alipotangaza azma ya kuwania muhula wa tatu, licha ya wasiwasi kuhusu uhalali wa hatua hiyo.
Umoja wa Ulaya na Amerika ziliweka vikwazo kutokana na ghasia hizo zilizogharimu maisha ya Warundi 1,200 na kupelekea 400,000 kuikimbia nchi hiyo, huku kukiwa na ripoti za kukamatwa kiholela, kuteswa, kuuawa na watu kutoweka kwa lazima.
Umoja wa Ulaya ulikuwa mfadhili mkuu kwa Burundi, na ilisema Jumanne iliamua kurejesha ufadhili kwa sababu ya “mchakato wa amani wa kisiasa ulioanza na uchaguzi mkuu wa Mei 2020 na ambao umeleta matumaini mapya kwa wakazi wa Burundi.”
Amerika ilifuata mkondo huo siku ya Ijumaa, kwa kile Burundi ilisema ni mpango wa msaada wa dola milioni 400 wa miaka mitano kwa ajili ya “maendeleo endelevu”nchini humo.
Burundi imekuwa katika hali mbaya ya kiuchumi tangu machafuko ya 2015, na ukosefu wa fedha za kigeni na kumekuwa na uhaba wa bidhaa muhimu kama vile mafuta, baadhi ya vyakula, vifaa vya ujenzi na madawa.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu wiki hii yamekosoa kuondolewa kwa vikwazo hivyo vya kimataifa, yakisema ukiukwaji bado unaendelea.
Kundi la haki la Ligue Iteka limeendelea kurekodi ukiukwaji mkubwa ikiwa ni pamoja na mauaji,watu kukamatwa kiholela na ukiukaji wa kijinsia unaofanywa bila kuadhibiwa, kulingana na taarifa ya muungano wa mashirika ya kiraia yaliyo uhamishoni.
Mnamo Septemba mwaka jana, Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa pia ilisema hali ya haki za binadamu imezorota tangu Ndayishimiye achukue mamlaka katikati ya mwaka wa 2020.