Mahakama Afrika Kusini Yafufua Mchakato Wa Kumuondoa Ramaphosa Madarakani

Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini imebatilisha kura ya Bunge la Taifa ya Desemba 13, 2022, iliyozuia kuanzishwa kwa mchakato wa kumwondoa madarakani Rais Cyril Ramaphosa kufuatia kashfa ya wizi wa fedha taslimu katika shamba lake.

Mahakama Afrika Kusini Yafufua Mchakato Wa Kumuondoa Ramaphosa Madarakani

Rais Ramaphosa alinusurika kwa urahisi kura hiyo ya Bunge mnamo 2022, wakati chama chake tawala cha African National Congress (ANC) kilikuwa na wingi wa wabunge. Ripoti ya jopo huru ilikuwa imehitimisha kwamba huenda rais alihusika katika makosa ya kimaadili, lakini wabunge waliikataa.

Jaji Mkuu Mandisa Maya alitangaza: “Kura ya Bunge la Taifa ya tarehe 13 Desemba 2022… hailingani na Katiba, ni batili, na imeondolewa.”

Uamuzi huo ulitokana na malalamiko ya chama cha upinzani cha mrengo wa kushoto, Economic Freedom Fighters (EFF).

Kashfa hii, maarufu kama Phala Phala Farmgate, ilihusisha takribani dola nusu milioni zilizokuwa zimehifadhiwa chini ya mito ya sofa katika shamba la ng’ombe na wanyamapori la Ramaphosa. Fedha hizo zinaripotiwa kuwa ziliibwa mwaka 2020. Ramaphosa alidai zilikuwa malipo ya mabeberu yaliyonunuliwa na mfanyabiashara kutoka Sudan.

Hata hivyo, alishtakiwa kwa kushindwa kuripoti tukio hilo kwa polisi, kutumia vibaya mamlaka yake, na kujihusisha na mgongano wa maslahi. Mwendesha mashtaka wa umma alifuta mashtaka hayo mnamo 2024.

Uamuzi wa Mahakama ya Katiba sasa unafungua njia ya kuanzishwa kwa uchunguzi wa kina wa kumwondoa rais madarakani, jambo linaloweza kuwa pigo kubwa kisiasa kwa Ramaphosa, hasa wakati ANC haina tena wingi wa wabunge bungeni.