Mahakama kuamua ikiwa Seneti itasikiza mashtaka dhidi ya Gachagua

Naibu Rais Rigathi Gachagua atafahamu leo Jumanne, saa 8:30 alasiri, ikiwa Bunge la Seneti litaendelea mbele na kikao cha kusikiza mashtaka dhidi yake.

Gachagua amewasilisha kesi mahakamani akipinga bunge hilo kuandaa kikao hicho.

Jaji wa Mahakama Kuu Chacha Mwita amepangiwa kutoa uamuzi juu ya pingamizi hiyo saa 8:30 alasiri leo Jumatano.

Bunge la Seneti limepangiwa kuandaa kikao cha Maseneta wote kesho Jumatano na keshokutwa Alhamisi ili kuangazia mashtaka 11 yaliyowasilishwa dhidi ya Gachagua kwa kusudi la kumbandua madarakani.

 

Hii ni baada ya Bunge la Taifa kupitisha hoja maalum ya kutaka Naibu huyo wa Rais kubanduliwa kwenye wadhifa huo ambao ameushikilia kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.

 

Hoja hiyo yenye mashtaka 11 iliwasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.

 

Miongoni mwa mambo mengine, Mutuse anamtuhumu Gachagua kwa kueneza semi za chuki, ukabila na kujilimbikizia mali kwa njia za kutilia shaka, mashtaka anayosema ni msingi tosha wa kumbandua Naibu Rais Madarakani.

 

Hayo yanajiri wakati ambapo Jaji Mkuu Martha Koome ameteua jopo la majaji watatu kusikiliza kesi ya kupinga kubanduliwa kwa Gachagua madarakani.

 

Jopo hilo lihahusisha Jaji Mkuu Eric Ogola na Majaji Anthony Mrima na Freda Mugambi.