Mahakama Kuu Yakataa Pingamizi La Jamhuri Katika Kesi Ya Uhaini Ya Tundu Lissu

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, leo Oktoba 13, 2025, imetoa uamuzi mdogo katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, kufuatia pingamizi lililowasilishwa na upande wa Jamhuri.

Mahakama Kuu Yakataa Pingamizi La Jamhuri Katika Kesi Ya Uhaini Ya Tundu Lissu

Wiki iliyopita siku ya Ijumaa tarehe 10, 2025 upande wa Jamhuri uliwasilisha pingamizi dhidi ya ombi la Lissu la kutaka kielelezo D1 maelezo ya maandishi ya shahidi wa pili wa Jamhuri, Inspekta wa Polisi John Kaaya, aliyoyatoa akiwa kituo cha polisi.

Mawakili wa Jamhuri walidai kuwa mshtakiwa hakufuata taratibu za kisheria katika kuwasilisha ombi hilo la kupokea kielelezo hicho kama ushahidi.

Hata hivyo, katika uamuzi wake uliotolewa leo, jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, limesema kuwa mshtakiwa ametimiza masharti yote ya kisheria yanayohitajika katika kuomba kielelezo hicho kipokelewe mahakamani.

Kutokana na uamuzi huo, Mahakama Kuu imetupilia mbali pingamizi la upande wa Jamhuri, na hivyo kielelezo D1 kinakuwa ushahidi wa kwanza kuwasilishwa na upande wa utetezi katika kesi hiyo ya uhaini inayoendelea leo mahakamani hapa.