Search
Close this search box.
East Africa

Mahakama ya juu nchini Kenya kutoa uamuzi kuhusu mpango wa BBI

9

Mahakama ya juu nchini Kenya Alhamis 31 Machi itatoa uamuzi kuhusu mabadiliko ya katiba yaliyopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta na washirika wake kabla ya uchaguzi muhimu mwezi Agosti.

Marekebisho hayo — ambayo yanajulikana kama Building Bridges Initiative (BBI) — yanalenga kupanua utendaji na yatakuwa badiliko kubwa zaidi katika mfumo wa kisiasa wa Kenya tangu kuanzishwa kwa katiba mpya mwaka wa 2010.

Jopo la majaji saba katika Mahakama ya Juu itafanya uamuzi kuhusu uhalali wa mapendekezo hayo kufuatia kukataliwa kwake mwaka jana na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, ambayo ilisema Kenyatta anaweza hata kushtakiwa katika mahakama ya kiraia kwa kuanzisha mchakato huo.

Kenyatta alikuwa amesema kuwa mpango huo wa BBI ungefanya siasa shirikishi zaidi na kusaidia kumaliza ghasia za mara kwa mara za baada ya uchaguzi katika taifa hilo.

Mbali na kuunda nyadhifa mpya katika ngazi za juu, mabadiliko hayo makubwa yangeongeza idadi ya wabunge kutoka 290 hadi 360.

Wapinzani wa BBI — akiwemo naibu rais William Ruto wanaona kuwa mpango wa BBI unatumiwa kumpa nafasi rais Uhuru Kenyatta kusalia madarakani.

Muda wa mageuzi hayo umezua uvumi katika miaka ya hivi karibuni kwamba Kenyatta anataka kusalia madarakani kwa kuanzisha wadhifa wa waziri mkuu kama sehemu ya BBI.

Naibu rais William Ruto, 54, alikuwa amependekezwa na Kenyatta kama mrithi wake lakini akajikuta akitengwa baada ya mapatano ya kushangaza ya 2018 kati ya rais na aliyekuwa hasimu wake Raila Odinga, ambao wana historia ndefu ya kupingana kwenye siasa.

Juhudi za wawili hao za kutaka BBI tangu 2018 zilizua uvumi kwamba Kenyatta anaweza kutwaa wadhifa mpya wa waziri mkuu katika mpango wa kugawana mamlaka iwapo Raila Odinga ,77, atashinda kiti cha rais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Mapema mwezi huu, Kenyatta, 60, aliimuidhinisha Odinga, ambaye atashindana na Ruto kuwania wadhfa wa urais.

Wachambuzi wanahoji kuwa uamuzi wa mahakama wa Alhamisi utavuruga misimamo ya kisiasa kati ya vyama vidogo, ambavyo vinazingatia chaguzi zao kabla ya uchaguzi wa rais na wabunge ikiwa imesalia miezi minne tu kabla uchaguzi mkuu.

Iwapo mahakama inayoongozwa na jaji mkuu wa kwanza mwanamke wa Kenya Martha Koome  itatoa uamuzi kuunga mkono BBI, Kenyatta na Odinga huenda wakajaribu kubadilisha katiba baada ya uchaguzi wa Agosti, wakili wa katiba Charles Kanjama alisema.

“Katiba haiwezekani kufanyiwa marekebisho kabla ya uchaguzi kwa sababu muda hautoshi, lakini suala la iwapo inaweza kurekebishwa pamoja na uchaguzi mkuu au mara baada… (inakuwa) wazi,” alisema.

Lakini “ikiwa mahakama itakataa mapendekezo hayo kwa sehemu au kwa ujumla, basi itatoa nafasi nzuri zaidi wa kisiasa kwa wale waliopinga mchakato huo.”

Comments are closed

Related Posts