Mahakama ya Namibia yakataa kutambua ndoa kati ya watu wa jinsia moja

Mahakama ya Namibia Alhamisi ilikataa kutambua ndoa kati ya watu wa jinsia moja zinazofanywa katika nchi nyingine, huku hakimu akionyesha huruma kwa wanandoa waliowasiluisha kesi ya mahakamani.

Wanandoa wawili waliooana nje ya Namibia walikuwa wameomba Mahakama Kuu kutambua ndoa zao.

Lakini jaji wa Mahakama ya Juu, Hannelie Prinsloo alisema amebanwa na uamuzi wa Mahakama ya Juu kutoka miongo miwili iliyopita ambao ulikataza ndoa za watu wa jinsia moja nchini Namibia.

Katika kutoa uamuzi huo wa kurasa 60, Prinsloo alisema anaamini kuwa Mahakama ya Juu ilikuwa na makosa, na aliweka hoja za kutambua ndoa kati ya mashoga.

“Mahakama ilituambia asubuhi ya leo, “tazama, tunataka kukusaidia, tunaamini kwamba unapaswa kufaulu katika masuala ya kikatiba,” wakili Carli Schlickerling alisema.

Wanandoa hao walitamaushwa na uamuzi huo lakini wakasema kuwa wangeomba Mahakama ya Juu kubatilisha uamuzi wake wa awali.

“Pengine tutaenda kwenye Mahakama ya Juu na kubadilisha uamuzi wa sasa wa Mahakama ya Juu ili uakisi haki,” alisema Anette Seiler, ambaye ameolewa na raia wa Ujerumani Anita Seiler-Lilles.

Walileta kesi hiyo pamoja na raia wa Namibia Johann Potgeiter na mume wake wa Afrika Kusini, Daniel Digashu.

Potgeiter na Digashu wana mtoto wa kiume (Lucas) mwenye umri wa miaka 13,aliyelelewa nchini Afrika Kusini.

Mtoto huyo alipewa fursa ya kuishi nchini Namibia katika kesi ya awali.

Namibia imeshuhudia msururu wa changamoto za mahakama kuhusu wapenzi wa jinsia moja kuoana, ikiwemo uzazi na uhamiaji.

Ushoga ni kinyume cha sheria nchini Namibia chini ya sheria ya ulawiti iliyoratibiwa mwaka wa1927.

Oktoba mwaka jana Mahakama Kuu ya Namibia ilitoa uraia kwa mtoto wa kiume wa miaka miwili wa wanandoa wa jinsia moja, na hivyo kumaliza vita vya kisheria juu ya ulezi na wazazi wa jinsia moja.