Mahakama ya Upeo nchini Kenya iliamua Alhamisi kwamba pendekezo lenye utata la Rais Uhuru Kenyatta kufanya marekebisho ya katiba si halali, na hivyo kuleta pigo kwake na washirika wake kabla ya uchaguzi mkuu mwezi Agosti.
Lakini iliacha wazi uwezekano wa mageuzi hayo — maarufu kama Building Bridges Initiative (BBI) — kuwasilishwa tena na bunge au kwa njia nyinginezo, mradi tu rais hahusiki katika mabadiliko hayo.
“Rais hawezi kuanzisha marekebisho ya katiba au mabadiliko kupitia mpango maarufu chini ya kifungu cha 257 cha katiba,” walisema majaji sita kati ya saba wanaosimamia kesi katika Mahakama ya Upeo.
Marekebisho hayo yangepanua mamlaka na kuongeza idadi ya viti vya ubunge katika mabadiliko makubwa zaidi ya mfumo wa kisiasa wa Kenya tangu kuanzishwa kwa katiba mpya mwaka wa 2010.
Mpango huo umewagawanya wasomi wa kisiasa nchini humo.
Kenyatta alikuwa amedai kuwa mabadiliko hayo yangefanya siasa kuwa shirikishi zaidi na kusaidia kumaliza misururu ya mara kwa mara ya ghasia za baada ya uchaguzi.
Uamuzi wa Alhamisi ulikuja baada ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa kutoa uamuzi dhidi ya marekebisho yaliyopendekezwa mwaka jana.
Mahakama ya rufaa ilisema Kenyatta anaweza kushtakiwa katika mahakama ya kiraia kwa kuanzisha mchakato huo.
Lakini Mahakama ya Juu iliamua kwa kauli moja dhidi ya wazo hili.
“Kesi za madai haziwezi kufunguliwa katika mahakama yoyote dhidi ya rais au mtu anayetekeleza majukumu ya afisi ya rais katika kipindi cha uongozi wake kuhusiana na jambo lolote lililofanywa au kutofanywa kwa mujibu wa katiba,” ilisema.
Wapinzani wa BBI — akiwemo naibu wa rais William Ruto — wanasema mpango wa BBI ulilenga kunyakua uongozi zaidi kwa rais ambaye hastahili kuwa uongozini kwa zaidi ya mihula miwili.
Muda wa mageuzi hayo ulizua uvumi katika miaka ya hivi karibuni kwamba Kenyatta alikuwa anataka kusalia madarakani kwa kuanzisha wadhifa wa waziri mkuu kama sehemu ya BBI.
“Ndoto imeahirishwa”
William Ruto, 54, alipendekezwa na Kenyatta kama mrithi wake, lakini akajikuta akitengwa baada ya mapatano ya kushangaza ya 2018 kati ya rais na aliyekuwa hasimu wake Raila Odinga, ambao wana historia ndefu ya kupingana kwenye siasa.
Juhudi za wawili hao za kutaka BBI tangu 2018 zilizua uvumi kwamba Kenyatta anaweza kutwaa wadhifa mpya wa waziri mkuu katika mpango wa kugawana mamlaka iwapo Odinga, 77, atashinda urais.
Mapema mwezi huu, Kenyatta, 60, alimuidhinisha Odinga, ambaye atashindana na Ruto kuwania kiti cha rais.
Kikao cha Alhamisi kilichukua muda wa saa sita, huku kila mmoja wa majaji akiwemo jaji mkuu wa kwanza mwanamke wa Kenya, Martha Koome, akisoma maamuzi yao mtawalia kuhusu kesi hiyo.
Wachambuzi wanasema uamuzi huo utaleta mkanganyiko wa kisiasa miongoni mwa vyama vidogo, ambavyo vinazingatia chaguzi zao kabla ya uchaguzi wa rais na bunge ambao umesalia miezi minne tu.
Kabla ya uamuzi huo, wakili wa katiba Charles Kanjama aliiambia AFP kwamba uamuzi ambao “unakataa mapendekezo hayo kwa sehemu au kwa ujumla… itawapa nafasi zaidi wa kisiasa wale wanaopinga mchakato huo.”
Ingawa uamuzi huo huenda ukadhoofisha ushawishi wa rais kabla ya uchaguzi wa Agosti, Kenyatta awali aliapa kuona mabadiliko ya katiba yakianzishwa katika maisha yake.
“Ingawa ilikumbana na vikwazo vya kisheria, naweza kusema tu kwamba BBI ni ndoto iliyoahirishwa,” Kenyatta alisema Desemba mwaka jana.
“Siku moja, siku moja, itatokea, kwa sababu nchi haiwezi kustahimili ubaguzi wa kikabila na kutengwa, kama vile haiwezi kustahimili uwakilishi usio wa haki na potofu. Hii ni kasoro ya muundo ambayo lazima turekebishe,” alisema.