Mahakama ya Rufaa ya Rwanda Jumatatu ilipitisha hukumu ya kifungo cha miaka 25 jela dhidi ya shujaa wa ‘Hotel Rwanda’ Paul Rusesabagina, ambaye alipatikana na hatia mwaka jana kwa tuhuma za ugaidi, na kukataa rufaa ya upande wa mashtaka ya kuongeza adhabu ya maisha.
Mkosoaji mkali wa Rais Paul Kagame, ambaye amekuwa rumande kwa takriban siku 600, alitiwa hatiani mwaka jana baada ya kesi ambayo familia yake na wafuasi wake walidai kuwa ilikuwa kesi ya mchongo na ukiukwaji wa sheria.
“Kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, mahakama inaona kwamba adhabu yake isiongezwe, kwa sababu miaka 25 aliyopewa inalingana na uzito wa makosa yake, na mahakama inashikilia adhabu yake,” alisema hakimu Francois Regis Rukundakuvuga.
Mahakama hiyo pia ilikuwa ikitoa uamuzi Jumatatu kuhusu rufaa dhidi ya hukumu zilizotolewa kwa washtakiwa 20 wa Rusesabagina, ambao walifungwa jela kati ya miaka mitatu na 20.
Washtakiwa wote walipatikana na hatia Septemba 2021 kwa kuunga mkono kundi la waasi lililojihami linalodaiwa kuhusika na mfululizo wa mashambulizi mabaya nchini Rwanda mwaka wa 2018 na 2019.
Rusesabagina mwenye umri wa miaka 67 amesusia kesi zote mahakamani na hakuwepo mahakamani kwa uamuzi wa Jumatatu.
Anasifiwa kwa kuokoa maisha ya zaidi ya watu 1,200 wakati wa mauaji ya halaiki ya 1994 nchini Rwanda, ambapo 800,000 wengi wao wakiwa Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani walichinjwa.
Lakini, katika miaka kadhaa baada ya Hollywood kumfanya kuwa mtu mashuhuri wa kimataifa, taswira tata zaidi iliibuka ya mkosoaji shupavu wa serikali ambaye hasira zake dhidi ya Kagame zilimfanya achukuliwe kama adui wa serikali.