Mahakama Yakataa Matumizi ya Kizimba cha Siri Hadi Kirekebishwe

Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo ya Dar es Salaam imekataa matumizi ya kizimba maalum kilichojengwa ndani ya chumba cha mahakama kwa ajili ya mashahidi wanaolindwa, ikielekeza kifanyiwe marekebisho kabla ya kuanza kutumika katika usikilizwaji wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Mahakama Yakataa Matumizi ya Kizimba cha Siri Hadi Kirekebishwe

Uamuzi huo umetolewa leo na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru, baada ya kusikiliza mapingamizi yaliyowasilishwa na mshtakiwa kuhusu uhalali wa kizimba hicho na utaratibu wa mashahidi wanaolindwa kutoa ushahidi.Akisoma uamuzi wa mahakama, Jaji Ndunguru alikumbusha kuwa Novemba 12, 2025, upande wa mashtaka walipomtambulisha shahidi wa nne anayelindwa P 11, mshtakiwa aliwasilisha mapingamizi matano, hatua iliyosababisha shahidi huyo kutoruhusiwa kutoa ushahidi hadi hoja hizo zitakaposikilizwa na kuamuliwa.

Katika pingamizi lake la kwanza, Lissu alipinga muundo wa kizimba hicho akieleza kuwa kinazuia hata majaji kumuona shahidi na kufuatilia mienendo na tabia zake wakati wa kutoa ushahidi, jambo alilodai linakiuka kanuni ya tatu ya ulinzi wa mashahidi.Mahakama ilikubaliana na hoja hiyo, ikieleza kuwa hata kama shahidi asingeibua hoja hiyo, mahakama yenyewe ingeona kuwa kizimba hicho, kwa jinsi kilivyojengwa, hakikidhi matakwa ya kisheria kwa kuwa kinawazuia majaji kumuona shahidi ipasavyo.Kutokana na hali hiyo, mahakama iliamua kuwa shahidi asitoe ushahidi ndani ya kizimba hicho hadi kitakapofanyiwa marekebisho.Katika pingamizi la pili, mshtakiwa alihoji namna mashahidi wanaolindwa walivyopatikana, akidai kuwa ni lazima mahakama ijiridhishe juu ya uhalali wao kabla ya kuruhusu wapewe ulinzi.Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, mahakama ilinukuu Kanuni ya 5(1), ya ulinzi wa mashahidi, inayoruhusu mahakama kutoa amri ya ulinzi iwapo itajiridhisha kuwa usalama wa maisha au mali za shahidi unaweza kuwa hatarini.Mahakama ilieleza kuwa amri ya ulinzi ilitolewa kwa kuzingatia masharti hayo ya kisheria, na hivyo pingamizi hilo halikuwa na msingi.Katika pingamizi la tatu, Lissu alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakuomba rasmi matumizi ya kizimba maalum, hivyo hakiwezi kutumika. Aidha, alieleza kuwa kufichwa kwa shahidi kunaweza kumzuia kumuhoji ipasavyo katika maswali ya dodoso.Mahakama ilisema ilipitia maombi ya ulinzi yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka na kubaini kuwa yaliomba mashahidi walindwe katika hatua za committal na usikilizwaji wa kesi (trial).Kwa mujibu wa mahakama, uwepo wa kizimba maalum ni sehemu ya utekelezaji wa amri ya ulinzi na hauwezi kuepukika katika mazingira ya shauri husika. Hata hivyo, ilisisitiza kuwa kizimba hicho lazima kiboreshwe ili kukidhi matakwa ya kisheria.Kuhusu hoja ya kushindwa kumuhoji shahidi, mahakama ilisema haijaona namna mshtakiwa atakavyoshindwa kuuliza maswali kwa sababu tu ya kutomuona shahidi uso wake, ikieleza kuwa kutofichuliwa kwa sura pekee hakutoshi kuonyesha kuwa haki ya maswali ya dodoso itakiukwa.-Jamhuri waomba ahirisho , Lissu apinga-Baada ya uamuzi huo, upande wa Jamhuri uliomba ahirisho la kesi, kutokana na maamuzi yaliyotolewa na Mahakama yamefanya shahidi wa siri waliyemuandaa kushindwa kuendelea kutoa ushahidi wake mpaka kizimba hicho kitakaporekebishwa.Hata hivyo, Lissu alipinga ombi hilo akieleza kuwa kuna ucheleweshaji usio wa lazima, akibainisha kuwa Serikali ina mashahidi 30, kati yao 11 wanaolindwa na 19 wasio na ulinzi.

“Mimi sina hatia, lakini ninaadhibiwa kwa ucheleweshaji huu,” alidai Lissu mahakamani.Lissu alieleza kuwa Serikali ina nafasi ya kuwaleta mashahidi wengine ili kuepusha ucheleweshaji wa kesi.Mara baada ya hoja hizo Mahakama iliamuru kizimba kwa ajili ya ushahidi wa siri kirekebishwe huku jopo la Mawakili wa Serikali wakitakiwa kuja na shahidi hapo kesho Alhamisi Februari 12, 2026, kwa namna mbili yaani shahidi wa siri na shahidi raia, ambapo ikiwa kizimba hakijamalizwa kurekebishwa basi shahidi wa kawaida ataendelea kutoa ushahidi na ikiwa kimekalika pia ushahidi utaendelea.

Lissu anaekabiliwa na kesi ya Uhaini alikamatwa Aprili 9,2025 mkoani Ruvuma muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara na kusafirishwa hadi Dar es Salaam, ambapo alifikishwa kwa mara ya kwanza Mahakama ya Kisutu Aprili 10,2025 na kusomewa mashtaka ya Uhaini.