Kesi kuhusu ujenzi wa kambi ya kifahari ya Ritz-Carlton Maasai Mara Safari Camp, iliyopo karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania, imechukua mkondo mpya baada ya Mahakama ya Ardhi na Mazingira kukataa ombi la kuifuta.
Kesi hiyo ilifunguliwa mwezi Agosti na mwanaharakati wa mazingira Meitamei Ole Dapash, aliyepinga kufunguliwa kwa kambi hiyo akidai imejengwa katika eneo muhimu la kupitisha wanyamapori kati ya Hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya na Hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania. Pia aliibua maswali kuhusu ulinzi wa mazingira, ushirikishwaji wa umma na haki za jamii za Wamaasai.
Katika hatua za awali za mgogoro huo, Dapash kupitia Taasisi ya Elimu, Utafiti na Uhifadhi wa Maasai (MERC) aliwasilisha barua ya madai kwa kampuni ya Marriott International, inayoendesha chapa ya Ritz-Carlton. Katika barua hiyo, aliomba maelezo kuhusu mikataba ya upangishaji wa ardhi, vibali vilivyotolewa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMA), pamoja na uthibitisho wa ushirikishwaji wa jamii za Wamaasai wakati wa kupanga na kujenga mradi huo.

Hata hivyo, Serikali ya Kaunti ya Narok ilikanusha madai hayo, ikisisitiza kuwa kambi hiyo ilijengwa kisheria na inafanya kazi kwa mujibu wa mkataba halali wa upangishaji. Viongozi wa kaunti hiyo walisema mradi unazingatia sheria za Kenya na mpango wa usimamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara na hauathiri mwenendo wa uhamaji wa wanyamapori. Serikali ya kaunti pia ilieleza kuwa mradi huo umechangia ajira, utalii wa kitamaduni na miradi ya kijamii kwa jamii zinazozunguka hifadhi hiyo.
Mnamo Jumatano Desemba 17, Dapash aliomba kuiondoa kesi hiyo, akieleza mahakamani kwamba mazungumzo na wahojiwa yalikuwa yameshughulikia masuala aliyoibua. Hata hivyo, msanidi wa mradi huo, Lazizi Mara Limited, alipinga ombi hilo, akidai kuwa kesi hilo linahusisha masuala ya maslahi ya umma na haliwezi kufutwa tu bila mapitio ya mahakama.
Jaji huyo alisema kuwa hoja hizo si za mtu binafsi pekee bali ni za maslahi ya umma, hivyo kesi haiwezi kusitishwa bila uchunguzi na uamuzi kamili wa mahakama. Mahakama imeelekeza kuwa kesi hiyo iendelee hadi itakapofikia hitimisho.
Kambi hiyo ya kifahari imeendelea kuwa gumzo katika ukanda wa Afrika Mashariki, hasa baada ya video kusambaa mitandaoni zikionyesha nyumbu wakionekana kuteseka karibu na eneo la mradi huo. Hata hivyo, Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya (KWS) lilikana madai hayo, likisema video hizo zilikuwa za kupotosha na kwamba kambi hiyo ipo katika eneo lililotengwa kwa uwekezaji wa utalii usioathiri mazingira kwa kiwango kikubwa.
Mahakama inatarajiwa kuendelea kusikiliza kesi hiyo huku ikichunguza iwapo mradi huo unazingatia kikamilifu sheria na masharti ya mazingira nchini Kenya.