
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, imekubaliana na pingamizi lililowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu na hivyo kukataa kupokea flash disk na kadi ya kumbukumbu (memory card) kama vielelezo katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji Dustan Nduguru ambaye anaongoza jopo la majaji watatu wanaosikiliza shauri hilo, wakati kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea kusikilizwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi kuhusu mapokezi ya vielelezo hivyo.
Katika hoja zake, Lissu ambaye anajitetea mwenyewe , aliiomba mahakama kutoruhusu vielelezo hivyo kupokelewa kwa maelezo kuwa shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Mkaguzi wa Polisi Samwel Kaaya (39), hana sifa za kitaalamu za kuwasilisha vielelezo vya picha za mjongeo kwani taaluma yake inahusu picha mnato pekee.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama imekubaliana na upande wa utetezi, ikibainisha kuwa shahidi huyo hana utaalamu unaohitajika kuthibitisha uhalali wa vielelezo vya video mahakamani.
“Mahakama imejiridhisha kuwa shahidi wa tatu si mtaalamu wa picha za mjongeo bali ni mtaalamu wa picha mnato, hivyo vielelezo vilivyowasilishwa haviwezi kupokelewa kama ushahidi,” alisema Jaji Nduguru akisoma uamuzi wa jopo la majaji watatu.
Kwa uamuzi huo, vielelezo hivyo flash disk na memory card havitatumika katika mwenendo wa kesi hiyo, ambayo inaendelea kusikilizwa Mahakamani hapo.