Mahamat Idriss Deby, kiongozi wa jeshi la serikali ya Chad, ametaja wabunge 93 wa bunge la mpito miezi mitano baada ya kujitangaza kuwa kiongozi wa nchi baada ya kifo cha babake, Rais Idriss Deby.
Kiongozi huyo wa jeshi alivunja bunge na kuahidi “uchaguzi wa huru na wazi” kwenye kipindi cha miezi 18 alipojitangaza kuwa mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Chad Aprili 20.
Wanachama wa upinzani wa zamani wa babake, ambaye pia aliingia madarakani mnamo 1990 akiwa mkuu wa kikosi cha waasi, ni kati ya wanachama wapya.Hakuna wawakilishi kutoka chama cha upinzani cha Wakit Tamma, au kutoka asasi za kiraia zilizopinga mapinduzi hayo ya Mahamat Idriss Deby.
Bunge la mpito NTC litakuwa baraza la mpito,kabla kufanyika kwa uchaguzi,hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari.
Mei 14, serikali ya jeshi ikiongozwa na Mahamat Deby na ikiwa na majenerali 14, ilimtaja Waziri mkuu wa zamani Albert Pahimi Padacke kuwa kaimu Waziri mkuu. Pahimi Padacke aliibuka wa pili katika uchaguzi wa urais wa Aprili 11 ambao Deby alishinda na kuwa rais kwa muhula wa sita.
Wiki moja baadae, Jeshi la Chad lilitangaza kuwa Deby ameuawa kutokana na majeraha aliyoyapata wakati alipokuwa akiongoza wanajeshi kwenye mstari wa mbele dhidi ya waasi wa Chad waliotaka kuuteka mji mkuu N’Djamena. Idriss Deby alaaga dunia akiwa na umri wa miaka 68.